Home Uncategorized LAZIMA TUJIFUNZE, MAANA SIKU TATU ZA BUNDESLIGA ZIMETUPA SIRI KIBAO

LAZIMA TUJIFUNZE, MAANA SIKU TATU ZA BUNDESLIGA ZIMETUPA SIRI KIBAO



Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema kama ni majibu ya jambo fulani wakati mwingine yanahitaji muda. Lakini siku mbili za Ligi Kuu ya Ujerumani au Bundesliga iliyokuwa imesimama kutokana na hofu ya Corona, kuna majibu ya maswali mengi tuliyokuwa tunajiuliza, yamepata majibu.


Pamoja na hayo yaliyopata majibu, bado kuna mengine yameibuka ambayo yanapaswa kuwa funzo kwa sehemu zote duniani ikiwemo Tanzania kwa kuwa mipango ya kumalizia ligi imekuwa sehemu ya mawazo.


Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamesema wamepeleka mapendekezo yao serikalini namna Ligi Kuu Bara inavyoweza kurejea na mechi 10 zimaliziwe.


Wakati tunasubiri nilieleza namna ambavyo Bundesliga ambayo imekuwa ligi kubwa na maarufu ya kwanza kurejea, tujifunze kupitia.

Kwa sasa Bundesliga ndiyo ligi maarufu zaidi duniani, kwa kipindi hiki inachezwa pekee. Nyingine zimesimama na ndiyo inaangaliwa na kila mpenda mpira lakini wakati imeanza kuchezwa juzi Jumamosi, jana Jumapili kabla ya kumalizia wiki yake ya kwanza leo. Hizo siku mbili zinatosha kabisa kuwa somo bora kwa wanaotaka kurejea lakini kwa wadau wote wa soka.


Wachezaji unfit:
Nilimuona Earling Haaland wa Borussia Dortmund akiwa amekaa chini, baadaye wachezaji kadhaa waliendelea kufanya hivyo.

Nikagundua kulikuwa na shida katika suala la utimamu wa mwili. Licha ya kwamba mwishoni walipata muda wa kujumuika pamoja lakini haikuwasaidia sana.

Kwa wachezaji wa hapa nyumbani Tanzania lakini pia makocha wanapaswa kuliona hilo mapema. Maana yake waongeze mazoezi na wajue kipi sahihi cha kufanya wawe fiti hasa.

Pamoja na hivyo kwa TFF na Bodi ya Ligi nao wajue kama watataka kurudisha ligi, mapema watoe nafasi kwa timu kupata muda wa kutosha wa mazoezi ili kutengeneza utimamu wa mwili kwa wachezaji.

Bila mashabiki, hovyo:
Acha mpira uchezwe katikati ya uwanja lakini mashabiki ndiyo kachumbari ya ladha ya mpira wenyewe. Angalia Bundesliga ndiyo ligi inayoendelea inayoongoza kwa kuingiza mashabiki wengi zaidi barani Ulaya, Borussia Dortmund ikiwa kinara kwa zaidi ya misimu mitatu.

Mechi za juzi na jana, zilikuwa utafikiri ni mazoezi na hii yote ni kutokana na kukosekana kwa mashabiki ambao wanakuwa “utamu” wa mpira kwa wale wanaoangalia kwenye runinga lakini pia kwa wachezaji wenyewe.

Unaona kabisa imesababisha hata mechi zenyewe kuwa na kasi iliyopungua kidogo. Hii inaonyesha mashabiki wanahitajika lakini kutokana na uhalisia, lazima kuwe na subira kwa kuwa afya ni muhimu.


Ladha imepotea:
Ndiyo ladha imepoteza, mtu akikosa hakuna zile kelele za “chips” jukwaani. Akifunga hakuna kelele za kushangilia lakini kwa sasa hakuna hata faida ya mwenyeji.

Kawaida mwenyeji hujivunia mashabiki lakini kwa sasa kila mmoja yuko ugenini, hivyo ni kuendelea kupambana kupata ushindi. Hii inapoteza ladha ya mpira kwa wachezaji wenyewe kama nilivyosema awali lakini hata kwa watazamaji katika runinga.

Kuna unafiki:
Inawezekana ni kutojiamini, siwezi kusema ni kuchukua tahadhari. Angalia mchezaji akifunga, hawasogeleani kushangilia lakini angalia wakati wanakabana wanakuwa karibu kabisa.

Nilikuwa najiuliza, kama wameshapimwa, vipi wasisogeleane tu? Maana majibu yametoka si wagonjwa vipi hofu iwe kubwa hivyo!

Angalia mchezaji akiwa katika benchi, anakaa mbali na wenzake kwa maana ya social distancing, lakini akiingia uwanjani wanaendelea kusogeleana. Binafsi naona kuna mambo mengine hata hayapaswi kuwepo ili kuendelea kupunguza hofu.

Kwanza ni msingi, vipimo sahihi na muda wa kutosha kupata majibu ili watu wakipata majibu, wanakuwa na uhakika na wanaweza kucheza mpira katika kile kiwango bora na chenye uhakika.

Tahadhari ni sahihi lakini isichukue nafasi kubwa hadi kufanya mpira unachezwa lakini hofu ndiyo inakuwa inayoendesha mchezo wenyewe.

Hata kama kiteknolojia wako juu yetu lakini tunaweza kujifunza kupitia Bundesliga na kuanza kufanya vitu vitakavyofanikisha Ligi Kuu Bara kurejea na itakapomalizika, kusiwe na wale walioumia kiafya kwa sababu ya maofisa tu kukosa umakini.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA YANGA KITAKACHOANZA LEO DHIDI YA TANZANIA PRISONS