Home Uncategorized MAONI YA WACHEZAJI WA NJE, ANGALIENI ISIJEKUWA ISHU YA MAJIBU MFUKONI

MAONI YA WACHEZAJI WA NJE, ANGALIENI ISIJEKUWA ISHU YA MAJIBU MFUKONI



NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na mjadala mkubwa kuhusiana na suala la Tanzania kubaki na wachezaji wa kigeni kwa idadi ya 10 au ipunguzwe.


Hii ni tokea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Felix Mwakyembe alipolieleza suala hili kuwa anaona wachezaji wa kigeni wapunguzwe ili kutoa nafasi kwa wazawa.


Baada ya hapo, wadau wengi wapenda soka walilipinga kwa nguvu kubwa sana suala hilo, hali iliyolilazimisha Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kutoa tamko.


Sehemu ya tamko la BMT lilikuwa ni kueleza kwamba kilichozungumzwa na Waziri Mwakyembe hakikuwa ni agizo badala yake ni kutoa nafasi kwa wadau wa soka kutoa maoni kuhusiana na suala hilo.


 Baada ya hapo ikaelezwa kwamba wadau watakutana pamoja na kupata nafasi ya kutoa maoni yao kuhisiana na suala hilo ili lifanyiwe kazi.


Siku chache baadaye nimeona BMT wakieleza kuwa wamekwama kuwakutanisha watu kwa pamoja na kutoa maoni kutokana na kipindi hiki cha mlipuko wa Corona kwa kuwa mikutano hairuhusiwi.


Hivyo, watakachofanya ni kuwapa nafasi wadau ya kutoa maoni kupitia mitandao ya kijamii pamoja na email.


Kwamba kama una maoni yako, wakaweka anuani ya email ya BMT ambayo unaweza kutuma maoni yako pale. Lakini wakatoa nafasi ya kutoa maoni yako kupitia mitandao hiyo ya kijamii.


Uamuzi huo wa BMT ni mzuri kwa kuwa wamelenga kuwapa nafasi wadau kutoa maoni yao lakini ukiuangalia unauona una walakini.


Kwanza, wakati waziri akizungumza kwa mara ya kwanza, sote tunajua halikuwa ni suala la maoni. Badala yake alizungumza kama jambo ambalo anataka kulifanyia marekebisho.


Pili, kupitia mitandao ya kijamii, hata kama watu watatoa maoni, tunaamini wana uelewa gani kuhusiana na mpira. Namna mambo yanavyoendeshwa kuhusiana na soka na wana utaalamu gani.


Hivi mfano, mashabiki tu wa kawaida, wakiamua kusema Tanzania ibaki na mchezaji mmoja wa kulipwa kutokana na ushabiki wao, labda uelewa wao mdogo kulingana na dunia inavyoendesha suala la wachezaji wa kigeni katika ligi mbalimbali, tutakubali!


Hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na maoni ya kishabiki tu badala ya maoni ya kitaalamu. Sikatai wadau wa kila aina kutoa maoni yao, lakini nashauri kuwepo kwa kamati ya wataalamu ambao watahusisha soka na utaalamu kama biashara na kadhalika.


Sote tunajua faida za wachezaji wa kigeni na hasara zake. Wapi Tanzania imefanya nini kupitia ilipokuwa na wachezaji wa kigeni au wachache na ninaamini Waziri Mwakyembe ana nia nzuri kabisa lakini bado anahitaji kujifunza suala hili kupitia wataalamu.


Kitu kingine ambacho nina hofu nacho isije ikawa tayari suala la nini kifanyike limepitishwa, halafu suala la watu kutoa maoni ikawa ni kama sehemu ya kisingizio hiki, haitakuwa sawasawa hata kidogo.


Wako watu wengi sana kama wataalamu ambao wana nafasi ya kulizungumza hili ikiwezekana kujadiliana na waziri mwenyewe na wataalamu wake lakini si kweli kila mmoja lazima aseme.


Kuna mambo mengi yanaweza kupitishwa au kufanyiwa kazi na yakawa na manufaa kwa ajili ya wengi lakini uamuzi wake ukawa umefanyika kupitia wataalamu wachache tu.


Si kila kitu lazima kipigiwe kura, si kila kitu lazima kila mmoja azungumze na suala la uhuru wa mawazo katika mambo ya kitaalamu linahitaji wataalamu au wadau wa karibu zaidi kuliko kila mtu.


Wanasema miluzi mingi humpotosha mbwa, hivyo tuangalie isije ikawa tunapita katika njia hiyo na ndio maana nashauri, iundwe kamati au kitu chenye wataalamu ambao watakaa na kujadiliana na watalaamu wa wizara na kadhalika katika kupata uamuzi mzuri katika hili.


BMT inapaswa pia kujua, kuna njia nyingi sahihi zaidi za kulishughulikia suala hili badala ya kutumia mitandao ya kijamii na kuna wepesi ya kuwafikia wadau wengi wa karibu lakini pia hata wataalamu wa BMT na wizara kwa ujumla, kujifunza kupitia ligi kubwa na maarufu duniani kama Premier League, Bundesliga, La Liga, Serie A, Ligue 1 wanafanyaje na hapa tukaangalia mazingira yetu yanasemaje lakini pia kurejea nyuma na kuangalia Tanzania yenye idadi kubwa ya wachezaji wa kulipwa na yenye idadi ya wachezaji wachache kwa kizazi cha sasa ilikuwaje.


Mfano, kuna sharti liliwahi kuzungumzwa kwamba kila mchezaji wa kigeni lazima awe anachezea timu yake ya taifa. Jiulize timu ngapi za Tanzania zina uwezo wa kununua wachezaji wa kigeni wanaocheza katika timu zao za taifa? Maana mchezaji anapoitwa timu ya taifa thamani yake inapanda. 

SOMA NA HII  LIGI USHINDANI NI MKUBWA, MASHABIKI TUIPE SAPOTI STARS