Home Uncategorized MTIBWA SUGAR WACHEKELEA TAMKO LA MAGUFULI

MTIBWA SUGAR WACHEKELEA TAMKO LA MAGUFULI


UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli anastahili pongezi kwa kuwakumbuka wanafamilia ya michezo kwa kuruhusu Ligi Kuu Bara kuendelea.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa wamelipokea kwa furaha tamko hilo jambo linalowafanya waanze kujipanga kurejesha timu kambini.
“Tulivunja kambi mapema, Machi 17 baada ya Serikali kuzuia masuala ya mijumuiko isiyo ya lazima kutokana na janga la Virusi vya Corona kwa kuwa tamko la Serikali limetolewa sasa tunaanza kujipanga kurejea upya.
“Magufuli ni mtu wa michezo baada ya kupewa ushauri kutoka kwa wataalamu wake ameona ni bora kurejesha burudani. Tunachosubiri kwa sasa ni ratiba kutoka Bodi ya Ligi ili kujua utaratibu utakwendaje,” amesema Kifaru.
Mei 21 Serikali ilitoa tamko la kuruhusu ligi zote kurejea ambapo itachezwa kwa vituo viwili vilivyopo Mwanza ambacho ni kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza na la Pili na Dar es Salaam itachezwa ligi kuu na Kombe la Shirikisho.
SOMA NA HII  SOLSKJAER: SARE NI KIPIMO CHA UWEZO WA WACHEZAJI WANGU