Home Uncategorized NIANZIE NA KELVIN KONGWE, ELIMU YA MENEJA INAHITAJIKA KWA WACHEZAJI WETU

NIANZIE NA KELVIN KONGWE, ELIMU YA MENEJA INAHITAJIKA KWA WACHEZAJI WETU





NA SALEH ALLY
JUZI usiku niliona beki wa kati wa Namungo FC, Paul Bukaba akiitambulisha kampuni mpya ambayo atakuwa akifanya nayo kazi zake.

Kampuni hii inajulikana kwa jina la Xzire ya nchini Misri na Bukaba beki wa zamani wa Simba atakuwa chini ya kampuni hiyo.

Baada ya kupata habari hiyo ya Bukaba nikaamua kufuatilia kampuni kadhaa za Misri kujua namna ambavyo zimekuwa zikifanya kazi, nikagundua zimekuwa na mafanikio makubwa lakini si yale ya jumla.

Kwamba kampuni zote za Misri zina mafanikio sana. Hata Xzire inajitahidi lakini haijawa kubwa sana lakini bado kwa Bukaba kama Mtanzania ni hatua.

Nasema hatua kwa kuwa nimeamua kulizungumzia suala la mchezaji kutakiwa kuwa na kampuni inayomsimamia na umuhimu wake.

Angalia wachezaji wakubwa pamoja na ukubwa wao lakini bado wanakuwa chini ya kampuni ambayo inaendesha mambo yake mengi.

Hapa tunapaswa pia kujifunza kwamba kuna tofauti kati ya kampuni ambayo inasimamia kazi za mchezaji na wakala. Kampuni kwa hapa nyumbani tunapenda kuita “meneja wake” lakini wakala yeye hatakiwi kuwa na mchezaji.

Kazi yake ni kusimamia makubaliano wakati wa mauzo ya mchezaji na anakuwa akifanya kazi kwa makubaliano na klabu na manajimenti ya mchezaji.

Wako mawakala wakubwa wao wamekuwa na kampuni ambazo wanafanya nazo kazi na wachezaji wanakuwa chini yao. Lakini pia kuna mikataba wanaweza kuingia ya kufanya kazi na wachezaji lakini si kuwamiliki kwa maana ya manajimenti.

Nilimsikia mshambuliaji nyota wa Kagera Sugar, Kelvin Kongwe Sabato, sisi tunamuita Kiduku akihojiwa na kusema angependa meneja wake amsaidie kuhakikisha anakula na kuendesha mambo mengine kwa kuwa hataki meneja awe anaonekana wakati anasaini mkataba.

Kauli yake ikanikumbusha rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa wakala lakini akapata wakati mgumu na wachezaji kwa kuwa walitaka yeye awe anawalipa mshahara.

Wachezaji kifedha hawahudumiwi na meneja au wakala, labda kama kuna ushikaji na kupozana. Meneja anasimamia mambo yake kama mchezaji kuhakikisha yanakwenda kwa usahihi.

Kama hakuna kulipana kwa asilimia wakati wa mauzo, mara nyingi mchezaji ndiye anapaswa kumlipa meneja. Kama sivyo, asilimia ya mauzo itakwenda kwa meneja ambaye pia anahusika kutafuta timu au mazingira mazuri ya mchezaji kikazi.

Mchezaji kazi yake inakuwa ni kucheza mpira na kuendelea kuipandisha thamani yake kwa kuonyesha kiwango bora zaidi.

Thamani yake inapopanda, mfano mshambulizi anafunga na kutoa asisti mfululizo, anamrahisishia meneja kazi yake na anaweza kumpatia timu kubwa zaidi au yenye malipo ya juu zaidi.

Nafikiri kuna haja ya hii elimu kuhusiana na mameneja au kampuni zinazosimamia wachezaji zinapaswa kufanya nini ili kuepusha migogoro kati ya wachezaji na mameneja au kampuni husika.

Mimi najua, kuna migogoro mingi sana kati ya wachezaji na kampuni au watu wanaowasimamia. Kwa kuwa wachezaji wanaamini meneja anapaswa awe anatoa mshahara, hili si jambo sahihi.

Meneja akiwa anafuata weledi hawezi kufanya hivyo labda kama kuna makubaliano ya ziada. Meneja ndiye anapaswa kulipwa na kama nilivyosema inategemea kama ni kwa asilimia au kila mwisho wa mwezi.

Ukisema leo Xzire ianze kumlipa mshashara Bukaba, basi labda wakati akianza kulipwa ikimtafutia timu ikate fedha zake.

Vizuri kwa wachezaji wa hapa waanze kutafuta makampuni ambayo yanaweza kuanza kufanya kazi ya kuwatangaza na kuwatafutia timu nje ya Tanzania.

Tuna wachezaji wengi wana uwezo lakini wanakwama kwa kuwa hawana watu wa kufanya kazi hizo ambao pia wana nafasi ya kuzuia sehemu ambazo klabu zinawabana wachezaji bila sababu za msingi au kuingia nao mikataba wanayokuwa hawajaielewa.

SOMA NA HII  WATU WAENDELEA KUCHOTA MIKWANJA YA MAANA KUTOKA SPORTPESA BONGO