Home Uncategorized ALICHOKISEMA EYMAEL KUHUSIANA NA YANGA KUTOMTUMIA TIKETI

ALICHOKISEMA EYMAEL KUHUSIANA NA YANGA KUTOMTUMIA TIKETI



Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael ameweka wazi kuwa hadi kufikia jana mchana uongozi wa Yanga ulikuwa bado haujamtumia tiketi ya ndege kuweza kurejea nchini kitu ambacho kimemkera.

Ligi inatarajia kuendelea Juni 13, mwaka huu huku Yanga ikicheza siku hiyo na Mwadui katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga bila kuwepo kwa kocha huyo ambaye bado amekwama nchini kwao.

Mbelgiji huyo aliondoka nchini baada ya Serikali kuzuia shughuli za kimichezo kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosambazwa na virusi vya Corona kabla kupungua kasi yake nchini na kuweza kurudisha shughuli za michezo kuanzia Juni Mosi, mwaka huu kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Taarifa za uhakika kutoka nchini Ubelgiji zinasema kuwa tayari serikali ya nchi hiyo imefungua anga lao tangu wikiendi iliyopita lakini bado kocha huyo ameendelea kubakia nchini huku timu yake ikiendelea na maandalizi ya ligi ikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa.
Chanzo hicho kilienda mbali zaidi kwa kusema kuwa kocha huyo amekuwa akifanya mawasiliano ya mara kwa mara na uongozi wa Yanga lakini bado umekuwa mgumu kumtumia tiketi ya ndege ya kurejea nchini jambo ambalo limeonyesha kumkera.
Championi lilimtafuta kocha huyo ambaye alisema kuwa mpaka sasa hajui anaweza kurejea nchini lini kwa kuwa uongozi wa timu hiyo umekuwa ‘ukimrusha’ juu ya suala la tiketi kadiri siku zinavyokwenda kwani anashindwa namna ya kuweza kufanya kazi yake akiwa mbali.
“Kiukweli sina furaha kabisa kwa sababu siwaelewi mabosi wangu kwa nini hawataki kunitumia tiketi ili niweze kuwahi timu kwenye maandalizi kabla ya mechi na Mwadui, sijui cha kufanya kwa kuwa inaninyima furaha.
“Unajua kama suala la ndege zimeshaanza kuruka hapa Ubelgiji tangu Jumamosi lakini nikiongea nao wao wanasema kesho yaani kila siku kesho ndiyo imekuwa kauli, angalia Simba imewarudisha wachezaji waliokuwepo nje, Azam pia kocha wake ametoka Ulaya, kwa nini mimi nishindwe kuja,” alisema Eymael.
Kocha huyo aliongeza kuwa: “Sijaona kama ni jambo sawa kwangu, nafanya kazi nikiwa mbali bila ya sababu za msingi, nimeongea na mwenyekiti lakini naye bado amekuwa hana majibu ya kueleweka, sasa sijui cha kufanya.”
Championi lilimtafuta Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, ambaye kwa upande wake alisema kuwa uongozi ulimtaka kocha huyo asafiri kwenda hadi Canada ili aweze kupata ndege ya moja kwa moja kurejea nchini lakini imekuwa ngumu kwake kutokana Ubelgiji kudai kuwa bado imefunga anga lake.
“Sisi tulimueleza mwalimu aende hadi Canada halafu huko atapanda ndege ya moja kwa moja kuja nchini lakini imekuwa ngumu kwa kuwa hakuna ndege ambazo zinatoka kwao,” alisema Nugaz.

SOMA NA HII  SHIME AWAPA TANO WACHEZAJI KUICHAPA UGANDA, MASHABIKI WAHUSIKA