Home Uncategorized JONAS MKUDE AFUNGUKA HALI YAKE ..AWAOMBA MASHABIKI KUMUOMBEA

JONAS MKUDE AFUNGUKA HALI YAKE ..AWAOMBA MASHABIKI KUMUOMBEA

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude amesema hali yake bado ni mbaya na kuwaomba mashabiki wake waendelee kumuombea ili afya yake iimarike.

Mkude aliumia juzi jioni na kupelekwa hospitali baada ya kukanyangwa na beki wa KMC, Kelvin Kijili katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Mo Simba Arena, Bunju. Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 3-1.

Kutokana na tukio hilo, Kijili amemuomba radhi kiungo huyo wa timu ya Taifa ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akisema haikuwa kusudio lake kumuumiza.

Kijili alisema tukio hilo lilitokea wapokuwa katika harakati za kuwania mpira, “niliudokoa, Mkude akapiga vidole chini ya meno ya njumu. Nia ilikuwa tuchukue mpira, mimi nikamuwahi, sikumchezea rafu, ‘niliuchopu’ bahati mbaya yeye akaingiza mguu kwenye meno, akapata shida kwenye vidole.”

Alisema hata yeye aliumia mguu wa kulia kwenye nyayo, lakini alijikaza na kuendelea na mechi kwani matukio kama hayo ndani ya uwanja huwa yanatokea.

“Niliumia lakini haikuwa kwa kiwango kikubwa kama Mkude. Nilipata maumivu kwenye nyayo za mguu wa kulia, nikajikaza hadi mechi ikaisha,” alisema, “nilikuwa kwenye mpango wa kutafuta namba yake ili nimpigie simu nimjulie hali, nimpe pole na nimwambie anisamehe kwani haikuwa kusudio langu kabisa kumuumiza na kuna maisha mengine nje ya mpira.”

Akizungumzia hali yake akiwa hospitali, Mkude alisema tangu alipoumia juzi amekuwa katika maumivu makali hadi jana alipokuwa akiendelea na matibabu Muhimbili.

“Niliumia vidole, bado nina maumivu makali ya mguu, ninaendelea na matibabu Muhimbili,” alisema Mkude kwa unyonge jana alipozungumza na Mwananchi.

Katika mchezo huo, mwamuzi Said Pambalelo alisimamisha pambano kuruhusu Mkude apatiwe huduma ya kwanza kabla ya madaktari wa Simba kumtoa nje na kuendelea kumpa huduma ya kwanza kisha kuita gari la wagonjwa lililompeleka hospitali.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema Mkude kwa hali yake, “tumetoa saa 72 za kusikilizia hali yake kabla ya kutoa taarifa zaidi ya maendeleo yake.”

SOMA NA HII  HUKO AZAM SIO POA UNAAMBIWA MASTAA HAWAMTAKI KOCHA.......HUKU MABOSI NAO WAZIBA MASIKIO