Home Uncategorized MASHABIKI MSIJISAHAU KWA FURSA MLIYOPEWA, MUHIMU KILA MMOJA KUCHUKUA TAHADHARI

MASHABIKI MSIJISAHAU KWA FURSA MLIYOPEWA, MUHIMU KILA MMOJA KUCHUKUA TAHADHARI


KUNA raha yake kushuhudia mechi ukiwa uwanjani. Miongoni mwa raha hizo ni kuwaona wachezaji wako moja kwa moja na wakati mwingine kuzungumza na kupiga nao picha kabla au baada ya mechi.
Ukiangalia kupitia runinga, unaikosa fursa hiyo ambayo hivi sasa nchi kadhaa wanaikosa.
Pia wachezaji nao wanaona fahari kucheza mechi huku jukwaani kukiwa na mashabiki wao. Wakati mwingine nguvu ya mashabiki kushangilia inawafanya wachezaji kupambana zaidi na kuipa timu ushindi.
Kukosekana kwa mashabiki viwanjani kuna mambo mengi yanatokea, klabu kukosa mapato, pia wachezaji ari kupungua kwa sababu huko nyuma walizoea nguvu ya mashabiki.
Tazama hivi sasa Ligi Kuu Hispania, England na hata Ujerumani, mechi zinachezwa bila ya mashabiki. Kuna ladha fulani imepotea hapo kati.
Zamani ukiingia pale Anfield, kama wewe timu pinzani kisha ukaona wale mashabiki wa Liverpool wanavyoimba kwa nguvu mwanzo mwisho, lazima uchanganyikiwe.
Lakini hivi sasa hakuna kitu kama hicho. Timu mwenyeji na ngeni zote zinaingia uwanjani bila ya mashabiki. Hapo nguvu ya mashabiki inakosekana na inaweza kuchangia timu kadhaa kupoteza mechi kirahisi.
Fursa ya mashabiki kuingia uwanjani hivi sasa baada ya kuwepo kwa janga la Corona, Tanzania tumeipata, nchi nyingi duniani hawajaipata kama hizo nilizozitaja hapo juu ingawa baadhi zao zinatumia njia mbadala kufanya kama vile mashabiki wapo.
Pale Hispania kuna sauti za mashabiki zinasikika, lakini pia kwa mbali kuna kama mashabiki wanaonekana pia, lakini uhalisia wake hakuna mashabiki viwanjani hii ni kutokana na kujikinga na Corona.
Kwa hapa nyumbani, Ligi Kuu Bara imerejea tangu Machi 13, mwaka huu, tumeshuhudia mechi kadhaa zikichezwa tena na mashabiki wakiruhusiwa kuingia viwanjani. Hii ni fursa ya kipekee kabisa.
Ligi hiyo imerejea ikiwa ni baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili kutokana na uwepo wa janga la Virusi vya Corona.
Kabla ya ligi hiyo kurejea, klabu zilipewa maelekezo pamoja na mashabiki vitu gani vya kuzingatia kutokana na uwepo wa Virusi vya Corona kwa kuchukua tahadhari.
Tumeshuhudia utaratibu mzuri kwa mashabiki katika baadhi ya viwanja na tahadhari ambazo wahusika wamekuwa wakizichukua.
Mashabiki wamejitahidi kufuata utaratibu kwa kuhakikisha wananawa mikono na kuvaa barakoa pindi wanapoingia uwanjani kutazama mechi zao.
Wachezaji nao pia wamekuwa wakifanyiwa vipimo kabla ya kuingia uwanjani na hii yote ni kuhakikisha wanaingia uwanjani wakiwa salama.
Lakini hapa kuna kitu mashabiki kama wanajisahau. Pengine ni mzuka wa kushangilia timu zao ambao wameuzoea tangu zamani.
Hivi sasa wanatakiwa kukaa kwa kuachiana nafasi, lakini mashabiki wanajisahau sana juu ya hiyo ishu.
Niliona katika mechi kadhaa ikiwemo ile ya Mwadui dhidi ya Yanga kwenye baadhi ya majukwaa mashabiki wamebanana sana, lakini pia katika mchezo wa hivi karibuni kati ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga kule Jamhuri, Dodoma.
Usisahau pia katika mechi ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting pale Uwanja wa Taifa, napo mashabiki baadhi walikaa jukwaani kwa kusogeleana sana ingawa si kwa kiwango kikubwa.
Hii ya Jamhuri kule Dodoma, ndiyo imekuwa funga kazi hadi kufikia hatua ya Serikali kutangaza kuanzia sasa kuwazuia mashabiki kuingia uwanjani wakati mechi zikichezwa hapo.
Pongezi kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kwani bado Corona ipo na tahadhari lazima zichukuliwe dhidi ya Virusi hivi hatari.
Mashabiki na nyie msijisahau, kwani mkiendelea na mtindo huu, mtaikosa hii fursa ya kwenda viwanjani, mtaishia kuziona timu zenu kupitia runinga hadi mwisho wa msimu.
SOMA NA HII  GALAS ATAJA KITAKACHOWAUMIZA WACHEZAJI LIGI KUU BARA ITAKAPOREJEA