SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Klabu ya Simba ambao ni mabingwa mara tatu mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18,2018/19 na 2019/20 amesema kuwa suala la yeye kutakiwa na Azam FC bado halijafika mezani.
Hivi karibuni ilielezwa kuwa Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba ipo kwenye hesabu za kuinasa saini ya Matola.
Matola ameweza kuzinoa timu nyingi kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na Lipuli FC ambayo alimaliza nayo ndani ya 10 kwa misimu miwili mfululizo ikiwa ni ule wa 2017/18 na 2018/19 kabla ya kusepa kikosini hapo kwa msimu wa 2019/20 na kuibukia Polisi Tanzania na sasa yupo ndani ya Simba.
Tayari Lipuli FC inayotumia Uwanja wa Samora imeshuka daraja na msimu wa 2020/21 itashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Akizungumza na Saleh Jembe, Matola amesema:”Mimi ni kocha wa Simba na ndipo ambapo ninafanya kazi kuhusu suala la kutakiwa na Azam FC sijapata taarifa na ikiwa watakuja nitazungumza.”
Azam FC kwa sasa inapambania kurejesha makali yake kwa kuwa msimu huu imeweka rekodi ya kuboronga kwenye mashindano yote iliyoshiriki.
Iliyeyeyusha taji la Kagame, taji la Mapinduzi,taji la Kombe la Shirikisho na lengo la kumaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi lilikwama pia.
Ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 70 baada ya kucheza mechi 38 nafasi ya pili ipo kwa Yanga yenye pointi 72.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa mpango mkubwa uliopo ni kuboresha kikosi kizima kwa ajili ya msimu ujao ikiwa ni pamoja na benchi la ufundi.