Home Uncategorized AGOSTI 14 MLIMANI CITY, BONDIA WA NGUMI KAONEKA ATAMBA KUWA AKIPIGWA NA...

AGOSTI 14 MLIMANI CITY, BONDIA WA NGUMI KAONEKA ATAMBA KUWA AKIPIGWA NA KIDUNDA ANAACHA NGUMI


BONDIA wa ngumi za kulipwa, Shabani Kaoneka anatarajia kupanda ulingoni katika pambano la raundi sita, uzito wa kati dhidi ya Seleman Kidunda ‘Mamba’ katika pambano litakalofanyika Agosti 14, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Kaoneka na Kidunda wao watakuwa kati ya mabondia watakaopanda ulingoni kwenye mapambano ya utangulizi ambayo yamedhaminiwa na Gazeti la Championi, Global Tv na Euromax.

Hiyo Agosti 14, kwenye Ukumbi wa Mlimani City na bado nchi ikiwa kwenye majonzi ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Willim Mkapa kutakuwa na vita kali ya kimataifa kati ya Mtanzania, Hassan Mwakinyo na Tshibangu Kayembe kutoka DR Congo.
Mwakinyo na Kayembe wao watakuwa wakigombania mkanda wa Dunia WBF katika pambano la raundi 12, uzito supa walter wakati Tony Rashid akitarajia kutetea ubingwa wake wa mkanda wa Afrika ‘ABU’ dhidi ya Mzimbabwe, Tinashe Mwadziwana katika pambano la raundi 12, uzito wa supa bantam.
Lakini ukiachana na hayo yote, Championi Jumatano limefanikiwa kufanya mahojiano na Shaban Kaoneka ambaye ataonyesha umwamba na Selaman Kidunda juu ya maandalizi yake kuelekea pambano hilo. Kaoneka ameanza kwa kusema kuwa: “Kwanza Kaoneka kama Kaoneka atabaki kuwa Kaoneka hilo mashabiki wanatakiwa walifahamu kwa sababu mimi ni mmoja kati ya mabondia wakali.
“Lakini najua siku ya Agosti 14, pale Mlimani City kuna watu watakuja na matokeo yao kutoka nyumbani ila nawaambia wasije na matokeo, waje kupata matokeo palepale ukumbini.

“Unajua mimi ni bondia mzoefu na mkubwa, nimecheza na Francis Cheka, Hassan Mwakinyo na marehemu Thomas Mashali hivyo nazijua vizuri ngumi na ngumi ni vita.
“Bondia ninayekwenda kukutana naye, nafahamu ni bondia mzuri kwa sababu amekwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya ngumi ila hata mimi siyo mnyonge nipo vizuri maana ngumi ni kazi yangu na maisha yangu.

“Kikubwa naomba mashabiki waje kwa wingi na waone nini kitakachotokea siku hiyo pale Mlimani City.

LABDA AHADI YAKO NI IPI KUTOKANA NA UBORA WA MPINZANI WAKO?
“Ninachoahidi mashabiki wangu kwamba kwangu hakuna KO, nawahaidi kwamba nitapigana mpaka tone langu la damu ya mwisho litoke. 

“Kikubwa niseme kwamba ikitokea nimepigwa nitakuwa nimeachana na mchezo wa ngumi yaani sitakuwa na sababu ya kuendelea kupigana ila nimejipanga kufanya vizuri.

“Mashabiki waje kuangalia ngumi kwa sababu najua mimi na Kidunda zitakuwa ngumi tamu, wasiwe na hofu waje kwa wingi .
INAONEKA UNAMCHUKULIA KIRAHISI MPINZANI WAKO?
“Sijasema kama mpinzani wangu ni bondia rahisi, namuheshimu ila kupigwa mimi ambaye nipo kwenye ngumi za kulipwa muda mrefu siyo rahisi maana najua kila kitu kwenye ngumi na ndiyo maana nimesema kama nitapigwa sina sababu ya kuendelea kucheza ngumi acha nikatafute michezo mingine.
KATIKA KIPINDI HIKI CHA MAANDALIZI RATIBA YAKO YA MLO IPOJE?
“Ukweli nakula ninachojisikia kwa sababu nje ya ngumi nafanya kazi ya kuajiliwa sasa siwezi kuwa na mlo maalum ila mara nyingi na kula sana ugali wa dona.

“Ipo hivi asubuhi nakula chapati zangu tano na supu halafu mchana ndiyo nusu ya ugali dona ndiyo maana hata ukiangalia mwili wangu unaonekana kuwa upo vizuri.
VIPI KUHUSU SUALA LA KUWA NA MENEJIMENTI?
“Kwanza sina menejimenti halafu mimi nafanya kazi kwa sababu huwezi kukaa na kitu ambacho hakiwezi kuingiza mfano leo pambano likiisha promota siwezi kumuona tena hadi litokee pambano lingine ila kazi yangu naenda kila siku nakutana na bosi, napata riziki,” anasema Kaoneka.

Mbali ya pambano hilo mengine yatakuwa ni kati ya Juma Choki atakayezichapa na Emanuel Mwakyembe wakati Baina Mazola akitarajia kumvaa Haidari Mchanjo.
SOMA NA HII  YANGA YAZIPIGIA HESABU POINTI TATU ZA BIASHARA UNITED