Home Uncategorized JAZBA UWANJANI WACHEZAJI TUZIPE KISOGO AFYA KWANZA

JAZBA UWANJANI WACHEZAJI TUZIPE KISOGO AFYA KWANZA

LIGI Kuu Bara msimu huu wa 2019/20 inatarajiwa kufikia tamati wiki ya mwisho ya mwezi huu ambapo hivi sasa timu zimebakiwa na mechi sita kutamatisha msimu.
Vinara Simba tayari wametangazwa mabingwa ambapo hivi sasa wana pointi 79 baada ya kucheza mechi 32. Yanga inashika nafasi ya pili na Azam ya tatu. 
Baada ya Simba kuwa mabingwa, Yanga na Azam zinapigana vikumbo kumaliza nafasi ya pili ambayo ni katika kuweka heshima tu kwa sababu nafasi hiyo haitawafanya kushiriki michuano ya kimataifa.
Nikukumbushe tu kuwa, kwa misimu ya karibuni mambo yamebadilika. Zamani timu ya kwanza na ya pili ndiyo zilikuwa na nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa. 
Lakini hivi sasa bingwa wa Ligi Kuu Bara na wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports ndiyo wanaiwakilisha nchi kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla sijafika mbali zaidi, nitumie nafasi hii kuwapongeza Simba kwa kufanikiwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni msimu wao wa tatu mfululizo. 
Kutwaa taji hilo huku zikiwa zimesalia mechi sita ni jambo zuri kwao na hii inaonesha wazi kwamba walijipanga kweli kufanikisha ishu hiyo.
Siku zote katika kufikia malengo, lazima uoneshe kweli mpambanaji. Ukiona Simba walivyoanza msimu huu walikuwa na moto kweli hadi wamefika hapo walipofika. 
Wapinzani wao, Yanga msimu huu waliteleza, sijajua tatizo kubwa lilikuwa nini ingawa mara kadhaa tuliona na kusikia matatizo ya wachezaji na viongozi wao.
Mafanikio ya Simba kwa msimu huu yawe chachu kwa wengine. Si Yanga na Azam pekee, bali kwa timu zote shiriki katika Ligi Kuu Bara. 
Msimu ujao ambao tutashuhudia timu 18 zikishiriki ligi hiyo, tunataka kuona ushindani ukiwa mkubwa zaidi. Hivi sasa Simba wanatamba kwamba watachukua tena taji hilo kwa misimu miwili mbele.
Tuachane na habari hizo za Simba kuwa bingwa. Tugeukie katika suala zima la nidhamu za wachezaji ndani ya uwanja. 
Watu wamekuwa wakisema kwamba mchezaji akiwa uwanjani, kadiri mchezo unavyozidi kwenda, basi damu inachemka na kufanya matukio ambayo mengine si ya kimichezo.
Kwa msimu huu tu tumeshuhudia matukio mengi ndani ya uwanja ambayo si ya kiungwana kabisa. 
Miongoni mwa hayo yamechukuliwa hatua ikiwemo kwa wachezaji Jonas Mkude, Bernard Morrison na Lamine Moro ingawa yapo mengi yametendeka.
Licha ya kwamba wachezaji wanapewa adhabu kwa yale ambayo huyafanya kutokana na hicho wanachosema kuwa na hasira, lakini kama hawasikii, wanaendelea kufanya tu. 
Tukio la hivi karibuni la kiungo wa Azam FC, Frank Domayo kumkanyanga beki wa Simba, Shomary Kapombe na kumsababishia maumivu makali.
Wapo wanaosema kwamba Domayo alifanya tukio hilo kwa makusudi, sitaki kuwa upande huo au upande wa kumtetea, lakini mwisho wa siku nasimamia upande wangu kwa kuwataka wachezaji kuacha michezo ya kihuni wanapokuwa uwanjani.
Hata kama una hasira kiasi gani, zuieni hizo hasira zenu kwani soka ni mchezo wa kiungwana, kila siku tunaimba huo wimbo kwani hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linawataka kufanya hivyo.

SOMA NA HII  JUHUDI YA WACHEZAJI YANGA YAMKOSHA KAZE