Home Uncategorized MORRISON AKINUKISHA TENA YANGA ADAI HAJALIPWA MKWANJA WAKE, UONGOZI WA YANGA WAFUNGUKA

MORRISON AKINUKISHA TENA YANGA ADAI HAJALIPWA MKWANJA WAKE, UONGOZI WA YANGA WAFUNGUKA


KIUNGO mtata wa Yanga, raia wa Ghana, Bernard Morrison amesema kuwa kwa sasa ni mchezaji huru hivyo anasubiria ruhusa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili aende kula bata la miezi miwili kwao.
Morrison alijiunga na Yanga kwenye dirisha dogo la Januari, mwaka huu, ambapo alionyesha kiwango cha hali ya juu ndani ya kikosi hicho jambo lililowafanya mashabiki wa Yanga kumpenda kabla ya kuingia kwenye mtafaruku wa mkataba wake.
Morrison ameweka wazi kwamba kinachomfanya aendelee kuwepo nchini hadi sasa ni TFF, ambao wamemtaka asubirie majibu ya madai yake ya utata wa mkataba na Yanga wanaodaiwa kumuongeza miaka miwili kabla ya ule wa miezi sita kuisha.

“Najua mashabiki wa Yanga, nimewakwaza sana, ila hilo halinisumbui sana maana ninachofanya ni kuhitaji haki yangu na kupunguza mambo ambayo yanataka kuniharibia maisha yangu.
“Kutokana na hilo sasa naisubiria TFF pekee inipe majibu yangu kisha nikapumzike kwetu Ghana.

“Sina mpango tena wa kurejea Yanga, maana uongozi siuelewi kabisa hadi leo hii nawadai mishahara yangu ya miezi miwili hawajanilipa.
“Sijui tatizo nini au ndiyo kisa cha kunilazimisha nimesaini mkataba wakati mimi natambua ule wa miezi sita tu, ngoja niende zangu Ghana nikapumzike,” alisema Morrison.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuhusu suala hilo alisema: “Nafikiri jambo zuri unalotakiwa kumwambia ni akupe slip zake za benki uone kama kweli anamaanisha, mwambie aache maneno yake ya ajabu.” 

Chanzo:Championi
SOMA NA HII  AJIBU AMERUDI,AFUNGA BAO LA KIDEO SIMBA IKISHINDA MABAO 3-1 MBELE YA KMC