Home Uncategorized WAKATI WA USAJILI, MIKATABA IWE MWONGOZO WA MAISHA YA BAADAYE

WAKATI WA USAJILI, MIKATABA IWE MWONGOZO WA MAISHA YA BAADAYE

NA SALEH ALLY

HUU ndio ule wakati uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka nchini, kipindi cha usajili.

Usajili umekuwa na kila aina ya gumzo kwa kuwa kila timu inakuwa katika mawindo ya kuwapata wachezaji fulani ili kujiimarisha.

Hapa ndipo huwa unasikia mchezaji fulani atajiunga na klabu fulani lakini ghafla unaambiwa imeshindikana amejiunga na klabu nyingine, ni kawaida kabisa.

Wakati unajua huyu anakwenda huku unasikia amekwenda kule, mwisho anasajiliwa kwingine. Hii ndio raha ya usajili, wasiolewa wakati mwingine wanaweza kuwa wanalaumu vyombo vya habari kwamba vimewaambia hivi lakini imekuwa tofauti lakini ni kawaida katika kipindi hiki.

Angalia, Ally Niyonzima au Awesu Awesu ilionekana ni chaguo la Yanga lakini wamekwenda Azam FC, Bakari Nondo Mwamnyeto ilionekana anatua Simba, Yanga wamemaliza kazi vizuri kabisa, huu ndio usajili.

Kipindi hiki hutokea mengi sana ambayo mwisho yanakwenda kuwa hadithi sababu raha iko hivi, klabu zinakuwa na uwanja mpana wa kuwapata wachezaji inaowahitaji.

Haya yote huwa ya kupita baada ya kila timu kupata inachokitaka kulingana na ilichokipata, baada ya hapo kitu muhimu kinakuwa ni namna ya kuendesha maisha kwa ufasaha.

Hapa ni ule mfano, kwamba kununua gari inaweza isiwe ishu kubwa sana lakini kuitunza kikawa kitu kigumu sana. Hivyo klabu lazima iwe na kitu ambacho kinaiunganisha na wachezaji kama muongozo namba moja wa maisha.

Kwangu naamini mikataba inapokuwa na ubora katika kuijenga tokea awali, inatengeneza muunganiko bora kabisa kati ya mchezaji na klabu.

Inakuwa hivi, wakati klabu inafanya usajili, bila shaka inakuwa inamtaka mchezaji kwa ajili ya kufaidika kwa maana ya kuisaidia kufikia malengo yake ya mafanikio na hapa ni utendaji bora wa kazi.

Bila shaka kabisa kwamba hata mchezaji naye atakuwa anategemea kupata mafanikio katika maisha yake kupitia kwa klabu hiyo kwa kupata mshahara na marupurupu sahihi kabisa, ili aendeshe maisha yake kwa ubora kabisa.

Sasa ili mambo yaende vizuri lazima kila mmoja atekeleze mambo yake kwa usajili ili kuwe na mafanikio na amani na mikataba ikiwa bora tokea mwanzo, basi ujue inatengeneza njia sahihi.

SOMA NA HII  MBABE WA YANGA AREJEA SIMBA

Mkataba utakuwa unaeleza kila kitu klabu itafanyaje linapofikia suala la malipo, mshahara ulipwe lini, marupurupu yawe vipi, mfano nyumba sahihi kwa mchezaji na kadhalika, pia uelezwe haya yote yatatekelezwa vipi.

Kwa upande wa mchezaji, hali kadhalika lazima kuwe na kipengele cha utendaji bora wa kazi wakati klabu inatekeleza mambo yake kwa ufasaha basi nayo ipate kilicho sahihi.

Isije ikawa mchezaji analipwa kwa wakati lakini haonyeshi juhudi na maarifa, hata kilichotarajiwa lakini bado klabu iendelee kumlipa kwa wakati tu na akichelewa analalamika wakati yeye hafanyi chochote, haiwezi kuwa sawa.

Pia haiwezekani klabu ikawa inadai mchezaji hajitumi, mchezaji mvivu wakati ana madai yake rundo na amepewa ahadi kibao ambazo hazijatekelezwa hata kidogo. Halafu mwisho inaishia kumuangushia tu lawama kwamba hajitumi au hafanyi lolote, haiwezi kuwa sahihi.

Mkataba unakuwa dira ya maisha ya pande zote mbili, ndio maana nasisitiza lazima uwe umewekwa kwa usahihi na hali inayoukumbusha kila upande kwamba jukumu lake kwenda upande mwingine liko hivi na lazima litekelezeke.

Kama yatatokea matatizo mengine basi kunaweza kukajadiliwa lakini mkataba ukabaki kuwa mwongozo sahihi.