Home Uncategorized PRINCE DUBE WA AZAM FC AWEKA REKODI YA KIBABE

PRINCE DUBE WA AZAM FC AWEKA REKODI YA KIBABE




PRINCE Dube, ingizo jipya ndani ya Klabu ya Azam FC ameweka rekodi ya kibabe kwenye mechi tatu alizocheza ambazo ni sawa  na dakika 270 Uwanja wa Azam Complex kwa kufunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Dube alianza kucheka na nyavu mara ya kwanza, Agosti 27 kwenye mchezo wa kirafiki mbele ya KMC alifunga bao hilo ndani ya 18 kwa guu lake la kulia akimalizia pasi ya kisigino ya Obrey Chirwa dakika ya 89.

Kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, Azam FC ilicheza na Polisi Tanzania, alimlipa deni ndugu yake Chirwa kwa kumtengenezea pasi ya bao wakati timu hiyo ikishinda bao 1-0, ilikuwa ni Septemba 7, alitoa pasi hiyo kwa guu lake la kushoto nje ya 18 ikakutana na ‘bichwa’ la Chirwa.

Aliendelea kuwasha moto Septemba 11 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union, alifunga mabao mawili, alianza kwa guu la kushoto dakika ya 68 akimalizia pasi ya Salum Abubakary na bao la pili alifunga dakika ya 89 kwa guu la kulia akimalizia pasi ya Oscar Masai.

Nyota huyo anaonekana kuwa mwiba akiwa ndani ya 18 kwa kuwa mabao yake yote matatu amefunga ndani ya 18 na uwezo wake mkubwa ni kutumia guu la kushoto, amefunga mabao mawili kwa mguu huo na bao moja amefunga kwa mguu wa kulia.

Agosti 17, Azam FC ilimtambulisha Prince Dube kutoka Zimbabwe, kwa dili la miaka miwili yeye ni mshambuliaji ambapo alijiunga na klabu hiyo akitokea Klabu ya Highlanders FC.

SOMA NA HII  LIVE: SIMBA 0-1 UD do SONGO