Home Uncategorized UONGOZI SIMBA WATAJA KILICHOWAPA TABU MBELE YA IHEFU FC,MBEYA, HESABU ZAO ZIPO...

UONGOZI SIMBA WATAJA KILICHOWAPA TABU MBELE YA IHEFU FC,MBEYA, HESABU ZAO ZIPO HIVI

 

UONGOZI wa Simba umesema kuwa ulitambua mchezo wa kwanza wa ufunguzi dhidi ya Ihefu ungekuwa mgumu kutokana na mazingira ya miundombinu ya Mbeya kutokuwa rafiki hivyo wamejipanga kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar. 

Septemba 6, Simba ilianza mbio za kutetea taji la Ligi Kuu Bara kwa kumenyana na Ihefu na ilishinda kwa mabao 2-1. Watupiaji kwa Simba ni John Bocco ambaye ni nahodha na Mzamiru Yassini huku lile la Ihefu likipachikwa na Omary Mponda.

Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa wachezaji walipambana kusaka ushindi ila mambo yalikuwa magumu kutokana na  Uwanja wa Sokoine kutokuwa rafiki.

“Najua mashabiki wanatambua namna Simba inavyocheza hivyo kwenye viwanja vile ambavyo vina matatizo kidogo inakuwa ngumu kuona Simba yenyewe lakini mwisho wa siku tumeshinda na kupata pointi tatu hilo ni jambo muhimu kwetu. 

“Kwa sasa hesabu zetu ni kuelekea mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar,  utakuwa mchezo mgumu utakaochezwa wikiendi ila tupo tayari,” amesema Manara. 

Mchezo huo utachezwa Septemba 12, Uwanja wa Jamhuri Morogoro ilipo ngome ya Mtibwa Sugar. Tayari Simba imeshawasili Dar, Septemba 7 kwa ajili ya kuanza kujiweka sawa kuelekea kwenye mchezo huo.

Simba inayonolewa na Sven Vandenbroeck inakwenda kukutana na Mtibwa Sugar inayonolewa na Zuber Katwila ambaye mchezo wake wa kwanza Septemba 6 alilazimisha sare ya bila kufungana dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Gairo.

SOMA NA HII  Safari ya Etiene kwenda Azam imetimia?