Home Uncategorized YANGA WATAJA MADENI YAO MAKUBWA MATATU

YANGA WATAJA MADENI YAO MAKUBWA MATATU


 KLABU ya Yanga imewaahidi mashabiki wake kuwa ipo kwenye mipango ya kuanza ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa timu hiyo utakaofanyika Kigamboni pamoja na uzinduzi wa duka la vifaa vya mazoezi na jezi mpya zitakazozinduliwa hivi karibuni.

 

Jumapili Yanga ilifanikiwa kuhitimisha siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi ambapo ilitambulisha wachezaji watakaotumika katika msimu wa mwaka 2020/21, katika siku hiyo Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi.

 

Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa viongozi wa timu hiyo wana madeni makubwa matatu ambayo ni ujenzi wa uwanja, uzinduzi wa duka pamoja na jezi mpya za timu hiyo.


“Tuna madeni matatu kwa Wanayanga ikiwemo jezi mpya, duka la vifaa, na ujenzi wa uwanja hivyo katika ujenzi wa uwanja tutakuwa na Kubwa Kuliko ambayo safari hii itakuwa kwa ajili ya mipango ya ujenzi wa uwanja huo ambayo utawezeshwa na Wanayanga wenyewe,” amesema Nugaz.

 

Kuhusu jezi amesema kuwa uzinduzi wa jezi utafanyika hivi karibuni na watautangaza uzinduzi huo na Yanga itakuwa timu ya kwanza kuzindua duka la jezi kwenye makao makuu ya klabu.


Kwa sasa Yanga ipo kwenye maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Septemba 6, Uwanja wa Mkapa dhidi ya Tanzania Prisons yenye maskani yake Sumbawanga.

SOMA NA HII  POLISI TANZANIA YAKATAA SARE YAKE DHIDI YA YANGA