KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amekiri kuwa ni kweli amekuwa akitofautiana mara kadhaa na baadhi ya nyota wengi wa kikosi hicho kutokana na maamuzi yake juu ya wachezaji gani wanaopaswa kuanza na wale watakaokaa benchi kwenye michezo yao.
Mwanzoni mwa msimu huu, Sven na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere walitajwa kuwa kwenye uhusiano mbaya kufuatia kocha huyo kumwanzisha benchi mchezaji huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo.
Sven amesema: “Nina furaha na kila mchezaji anayeunda kikosi changu, hii inajumuisha hata wale ambao hawachezi mara kwa mara, kwa bahati mbaya kwenye kila mchezo ni wachezaji 18 pekee ambao wanakuwa kwenye listi na wachezaji wengine kumi hawapati kabisa nafasi ya kuwa sehemu ya mchezo.
“Kuna wakati ninapofanya maamuzi ya wachezaji gani watacheza wapo baadhi ya nyota ambao hukasirishwa na hilo na mara kadhaa hubaki wakiwa na hasira kwa siku nzima lakini jambo zuri ni kuwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo nao wanaelewa kuwa hali hii ni ya kawaida na ni lazima itokee.”
Hata hivyo ukiangalia rekodi za msimu uliopita na huu wa sasa utabaini kuwa Kagere ni mshambuliaji tegemeo kikosini hapo.
Katika mechi nne za kwanza za ligi msimu uliopita Simba ikiwa chini ya Kocha Patrick Aussems, Kagere alicheza dakika zote na alifanikiwa kufunga mabao sita, msimu huu chini ya Sven ameanza kwenye michezo mitatu na miwili akitokea benchi ambapo amefunga mabao manne.