Home Uncategorized KABLA YA YANGA NA SIMBA, MECHI ZAO ZA MOTO HIZI HAPA

KABLA YA YANGA NA SIMBA, MECHI ZAO ZA MOTO HIZI HAPA


NOVEMBA 7, Uwanja wa Mkapa ile mechi ambayo iliota mbawa Oktoba 18  sasa inatarajiwa kupigwa kwa watani hawa wa jadi kuweza kukutana ndani ya uwanja.

Kuelekea mechi hiyo timu zote zimebakiwa na mechi nne mkononi za kucheza ambazo ni dakika 360, katika mechi hizo, Simba itacheza mechi tatu Dar na moja itapigwa nje ya Dar na Yanga itacheza mechi tatu nje ya Dar na moja itachezwa Dar.


Cheki vigongo vinne kwa vigogo hawa ndani ya ligi kabla ya kukutana mambo yatakwenda namna hii:-

 

Yanga v Polisi Tanzania


Mchezo wa sita kwa Yanga msimu wa 2020/21 ikiwa na pointi 13 na inakutana na Polisi Tanzania  iliyo nafasi ya 7 ikiwa na pointi 10. Itakuwa Oktoba 22.

Kigongo hiki kitakuwa Uwanja wa Mkapa.Timu zote mbili mechi zao zilizopita zimeshinda. Yanga ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkapa na Polisi Tanzania ilishinda bao 1-0 dhidi ya KMC, Uwanja wa Uhuru.

 

KMC    vs   Yanga                           


Hii itachezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Oktoba 25.Kwa sasa KMC imeonekana kuwa imara kwenye safu yake ya ushambuliaji kwenye mechi zake tano imefunga mabao nane na tatizo lake lipo kwenye safu ya ulinzi ambayo imefungwa mabao manne.


Yanga ina rekodi nzuri kwenye mechi zake za ugenini msimu huu ikiwa imecheza mechi mbili ilishinda zote mbele ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kote ilishinda bao 1-0.Safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao saba na ulinzi imeruhusu bao moja.



Biashara  vs    Yanga                                 


Moja ya kigongo kikali kwa Yanga itakuwa dhidi ya Biashara United Uwanja wa Karume. Biashara  United nyumbani wamekuwa na balaa.

Mechi nne, zote wameshinda. Tatu walicheza Uwanja wa Karume na kufunga mabao matatu na hawakufungwa. Moja walicheza Uwanja wa Kirumba na ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.


Inakutana na Yanga Novemba Mosi kusaka pointi tatu.

 

Gwambina   vs    Yanga

               

Yanga itakutana na mbinu za kocha wao wa zamani, Mwinyi Zahera ambaye yupo kwenye benchi la ufundi akiwa ni mkurugenzi ndani ya Gwambina FC ambayo imepanda daraja msimu huu.


Kazi kubwa itakuwa kwa timu zote kusaka rekodi mpya ndani ya ligi kwa kuwa ni msimu wao wa kwanza kukutana ndani ya Ligi Kuu Bara. Itakuwa ni Novemba 3, CCM Kirumba.



Vigongo vya Simba


Prisons   vs  Simba                                   

 Simba inarudi Rukwa kwa mara ya pili baada ya kuanza kutwaa Kombe la Shirikisho ilipocheza na Namungo FC kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.


 Oktoba 22 ambapo Tanzania Prisons itawakaribisha Simba. Mwendo wa Prisons msimu wa 2020/21 kwenye mechi tano imeshinda mechi moja na ina sare mbili sawa na idadi ya mechi ilizopoteza.

Ikiwa nafasi ya 12 na pointi tano inakutana na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi zake 13 kibindoni.

SOMA NA HII  GAMONDI AFANYA MAAMUZI HAYA MAMBO YAISHE

 

Simba  vs  Ruvu Shooting             

 

Baada ya kumalizana na wajeda wa Prisons, Simba inakutana na wajeda wengine, Ruvu Shooting yenye sera ya kupapasa.  Ni Oktoba 26, Uwanja wa Mkapa.



Ruvu Shooting ikiwa imecheza mechi sita imeshinda mechi mbili dhidi ya Gwambina FC kwa kufunga bao 1-0  na mbele ya JKT Tanzania kwa ushindi wa bao 1-0 na imepoteza mechi mbili na kupata sare mbili. Safu ya ushambuliaji imefunga mabao mawili na ile ya ulinzi imefungwa mabao matatu kibindoni.


Ipo chini ya Charlse Mkwasa ambaye alimpa tabu kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alipokuwa akikinoa kikosi cha Yanga, Januari 4, kwenye sare ya kufungana mabao 2-2.

 

Simba vs Mwadui        


Mabingwa watetezi Simba watasalia Dar tena na watashuka uwanjani Oktoba 31 watakapomenyana na Mwadui FC,Uwanja wa Mkapa.


Rekodi zinaonyesha kuwa mchezo wa kwanza kwa msimu wa 2019/20 kupoteza kwa Simba ilikuwa mbele ya hawa jamaa, mchezo ulichezwa Uwanja Kambarage, Shinyanga. Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.


2020/21 haijawa na mwendo mzuri Mwadui FC licha ya kwamba imeshinda mechi mbili mfululizo mbele ya Namungo FC kwa bao 1-0 na Ihefu kwa mabao 2-0 ipo nafasi ya 11 na kibindoni ina pointi 6.Inakutana na Simba  ambayo imeshinda mechi tatu mfululizo ilikuwa ni mbele ya Biashara United mabao 3-0, Gwambina mabao 3-0 na JKT Tanzania mabao 4-0.

  

Simba   vs  Kagera Sugar                  


Kabla ya Novemba 7 kufika, Simba itamalizana na Kagera Sugar ya Mecky Maxime mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.Itakuwa ni Novemba 4.


Kikwazo kikubwa kwa Maxime ni safu yake ya ushambuliaji kwa kuwa ikiwa imecheza mechi sita imefunga mabao manne na ile ya Simba imefunga mabao 14. Kinara wao ni Yusuph Mhilu ambaye amefunga mabao mawili na moja limefungwa na beki, David Luhende.

Safu ya ulinzi ya Kagera Sugar imeruhusu kufungwa mabao nane inakutana na ile ya Simba iliyo chini ya Joash Onyango ambayo imefungwa mabao mawiili na Uwanja wa Mkapa bado haijaokota mpira nyavuni.

 

Yanga  v Simba

 

Baada ya watani hawa kukamilisha safari yao ya dakika 360 sasa ngoma itakuwa Novemba 7, Uwanja wa Mkapa.


Mabao matano yalikusanywa msimu wa 2019/20 kwa wababe hawa walipokutana ndani ya uwanja. Mchezo wa kwanza uliochezwa Januari 4, Simba ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na ule wa pili uliochezwa Machi 8, Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Walipokuwa wakisaka pointi sita, Yanga ilibeba pointi nne na kufunga mabao matatu huku Simba ikiambulia pointi moja na mabao mawil Novemba 7 itakuwa ni mechi yao ya kwanza kwa msimu wa 2020/21 baada ya Oktoba 18 mechi yao kuyeyuka mazima.

Dakika 90 zitaamua nani awe mshindi kwenye mchezo huu ambao umechukua hisia za wengi.