Home Uncategorized NYOTA HAWA WALITISHA RAUNDI YA NNE

NYOTA HAWA WALITISHA RAUNDI YA NNE


NGOMA bado hailali kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa ni raundi ya nne na mambo yanazidi kupamba moto kila raundi na rekodi zake.

Ushindani mkubwa unafanya kila mchezaji kupambana kuandika rekodi zitakazoifanya timu yake kufikia mafanikio.

Azam FC wao kwa raudi ya nne ni vinara wameishusha KMC ambayo ilidumu kwenye nafasi hiyo kwa raundi tatu, hawa hapa nyota ambao waliweza kutisha raundi ya nne:-        

Meddie Kagere

Balaa la Gwambina Uwanja wa Mkapa mbele ya Simba lilikwama dakika ya 40 kupitia kichwa cha Kagere ambaye alipachika bao lake la pili kweye ligi.

Bao lake la kwanza alipachika raundi ya tatu wakati Simba ikishinda mabao 4-0 mbele ya Biashara United. Ameanza kuifukuzia rekodi yake ya mabao 22 ambayo alifikia msimu wa 2019/20 na kutwaa kiatu cha ufungaji bora.

Prince Dube

Mtupiaji namba moja ndani ya ligi ni Dube kibindoni ana mabao matatu na pasi moja ya bao. Aliweza kufunga bao lake la tatu mbele ya Tanzania Prisons wakati timu yake ikishinda bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela.

Mabao yake mawili alifunga mbele ya Coastal Union ilikuwa raundi ya pili huku pasi yake ya kwanza aliitoa kwa Obrey Chirwa raundi ya kwanza wakati Azam FC ikishinda bao 1-0. Jumla Azam FC imefunga mabao matano huku yeye akihusika kwenye mabao manne.

David Kissu

Kipa namba moja wa Azam FC, Kissu raundi zote nne amekuwa imara kulinda nyavu zake zisitikiswe.

Alianza mbele ya Polisi Tanzania wakati Azam FC ikishinda bao 1-0, Azam 2-0 Coastal Union na mbeya City 0-1 Azam FC. Raundi ya nne alikamilisha dakika zake 360 bila lango lake kuguswa huku timu yake ikiwa ni namba moja kwenye msimamo na pointi 12 kibindoni.

Luis Miqussone

Hajajenga ushkaji na nyavu kwa msimu wa 2020/21 ila yupo nyuma kwa wale ambao wanajenga ushkaji na nyavu. Wakati Simba ikishinda kwa mabao 3-0 mbele ya Gwambina alipiga kona iliyokutana na kichwa cha Kagere kilichomshinda mlinda mlango wa Gwambina FC, Mohamed Makaka.

Jumla ana pasi nne za mabao ndiye kinara kwa sasa ndani ya ligi.

Mussa Mbissa

  Wakati Fred Felix akipachika bao la kwanza dakika ya 6 na Wallace Kiango akiandika bao la pili dakika ya 37, mlinda mlango namba moja wa Mwadui FC, Mbissa aliweza kuondoka na ‘clean sheet’ yake ya kwanza ndani ya ligi.

SOMA NA HII  KOEMAN ARITHI MIKOBA YA SOLAR ALIYECHAPWA MABAO 8-2 LIGI YA MABINGWA ULAYA

Ushindi wa kwanza pia kwa Mwadui ambayo ilicheza mechi tatu ndani ya dakika 270 na kufungwa mabao manne ilikuwa mbele ya Biashara United 1-0 Mwadui, Mwadui 1-2 KMC na Dodoma Jiji 1-0 Mwadui. Ila mzunguko wan ne aliweza kuwa shujaa mbele ya Ihefu FC.

Chris Mugalu

Amekuwa na ushkaji mkubwa na nyavu akiwa amefunga mabao mawili ndani ya ligi. Alianza kuwatungua Biashaa United Uwanja wa Mkapa wakati Simba ikishinda mabao 4-0 ilikuwa raundi ya tatu na raundi ya nne alipachika bao lake la pili Uwanja wa Mkapa wakati Simba ikishinda mabao 3-0.

Alitumia dakika 14 mbele ya Biashara United na dakika 16 mbele ya Gwambina na kumfanya atumie jumla ya dakika 30, ana wastani wakuwa na hatari kila baada ya dakika 15.

Lamine Moro

Beki kisiki ndani ya Yanga, mechi zake tatu ambazo ni dakika 270 Yanga haijaruhusu bao, amefunga mabao mawili ilikuwa wakati Yanga ikishinda bao 1-0 mbele ya Mbeya City na bao lake la pili alifunga raundiya nne alifunga mbele ya Mtibwa Sugar kwenye ushindi wa bao 1-0.

Yanga ikiwa imefunga mabao mabao manne kibindoni nusu yake ameyatupia Moro kwa kuwa ana mabao mawili.

Carlos Carlinhos

Amepewa jukumu la kupiga mipira iliyokufa ndani ya Yanga. Mechi yake ya kwanza kuanza kipindi cha kwanza ilikuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati Yanga ikishinda bao 1-0.

Alitumia dakika 72 uwanjani na dakika ya 61 kwenye mzunguko wa nne alitoa pasi ya bao kwa Lamine Moro na kumfanya awe kinara wa pasi za mwisho ndani ya Yanga kwa kuwa alifikisha pasi yake ya pili.  

Marcel Kaheza

Nyota huyu wa Polisi Tanzania anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye raundi ya nne ambapo alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Dodoma Jiji.

Ameanza kuonyesha makeke yake ambapo msimu uliopita nyota huyo alitupia jumla ya mabao tisa kibindoni.

Yusuph Mhilu

Mzawa ambaye alikuwa moto kwa msimu wa 2019/20 ndani ya ligi kwa kucheka na nyavu amerejea kwa kasi ambapo raundi ya kwanza mpaka ya tatu hakupata nafasi ya kucheza.

Mchezo wake wa kwanza ulikuwa ni wa raundi ya nne ilikuwa mbele ya KMC ambao walikuwa wamecheza mechi tatu bila kupoteza. Aliwatungua bao moja na kufungua akaunti yake ya mabao na msimu uliopita alifunga mabao 13.