Home Uncategorized TAIFA STARS: TUNAWEKA REKODI KESHO KWA MKAPA

TAIFA STARS: TUNAWEKA REKODI KESHO KWA MKAPA


 SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, amesema kuwa wataandika rekodi mpya Uwanja wa Mkapa kwa kupata ushindi ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kucheza baada ya uwanja huo kubadilishwa jina kutoka Uwanja wa Taifa na kuitwa Benjamini Mkapa.

Kesho, timu ya Taifa ya Tanzania inayonolewa na Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije itakuwa na kazi ya kufanya Uwanja wa Mkapa kwa kucheza mchezo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa dhidi ya Burundi.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Matola alisema kuwa timu iliwahi kuingia kambini Oktoba 5 na mazoezi walianza Oktoba 6 jambo linalowafanya waamini kwamba watafanya kweli kwenye mchezo huo.

 “Tuko tayari kwa ajili ya mechi ya jumapili, haitakuwa mechi rahisi. Ukichukulia Burundi ni timu ambayo tuliiondoa katika kufunzu Afcon. Tumejiandaa tupate matokeo katika mchezo wetu.

“Tunajua kuwa Warundi sio watu rahisi na kweli wameleta wachezaji wao kutoka nje na sisi tumeleta wachezaji wetu kutoka nje. Tutamkosa John Bocco kwenye mchezo huo kwa kuwa tulimruhusu arudi nyumbani kwa ajili ya matibabu, alijiunga na timu akiwa bado ana majeruhi aliyoyapata katika klabu yake ya Simba. Himid Mau ataingia leo (jana),” alisema Matola.

Kwa upande wake nahodha msaidizi wa Stars, Aishi Manula alisema :-“ Kwa niaba ya wachezaji tuko tayari kwa ajili ya kupambana na majirani zetu. Mara zote tukicheza nao, mechi huwa ni ngumu na ya ushindani, ila hii itakuwa mechi ambayo tutapigana kwa jasho na damu

“Kuupa uwanja wetu wa taifa, jina la mzee Mkapa kwa ajili ya kumuenzi yeye na mambo makubwa aliyofanya, ni heshima kwetu sisi wachezaji. Kwa heshima ya baba yetu, tunaahidi kufanya mambo makubwa zaidi na kuupa heshima zaidi uwanja wetu wa Mkapa”, alisema Manula.

Naye Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Burundi, Jimmy Ndayizeye alisema kuwa,tulikuwa na maombi ya mechi tatu za kirafiki, ila tulichagua Tanzania, kwa sababu Tanzania na Burundi ni ndugu. Wachezaji wetu wako tayari na mmoja wa mwisho atawasili leo (jana).

SOMA NA HII  VPL:YANGA 0-0 MBEYA CITY