Home Uncategorized WACHEZAJI WAKATI HUU NI MUHIMU KUONGEZA JUHUDI ILI KUJIWEKA SOKONI

WACHEZAJI WAKATI HUU NI MUHIMU KUONGEZA JUHUDI ILI KUJIWEKA SOKONI


 

LIGI Kuu Bara imekuwa na changamoto kubwa hasa kwa upande wa waamuzi pamoja na wachezaji wenyewe kushindana ndani ya uwanja huku suala la kufungia viwanja nalo likiwa linazidi kuibuka kila iitwapo leo.

Mechi nyingi ambazo zinachezwa zimekuwa na ushindani mkubwa jambo ambalo linaleta mvuto wa kuzitazama na kuzifuatilia.

Tunachokihitaji ndani ya ligi kwa sasa ni ushindani kwa sababu kukiwa na ushindani kunafanya kila timu iamini kwamba ipo imara na inaweza kuleta ushindani kwa mpinzani.

Ushindani utasaidia kukuza ligi na kufanya kuwe na timu ya Taifa ya Tanzania ambayo ni imara na itaweza kufanya vema kwenye michuano mbalimbali kimataifa.
Jambo hilo litasaidia kuuza wachezaji wa ndani nje ya nchi jambo ambalo litafanya soka letu kuwa bora na kuzidi kuleta ushindani kwa mataifa mengine ambayo yameendelea.

Ili kuwa na ligi makini pamoja na timu ya Taifa bora ni lazima uwe na wachezaji wengi ambao wanajituma na kufanya vizuri ndani ya uwanja.
Kwa kufanya hivyo ikiwa itatokea wachezaji wengi 

watauzwa nje ya nchi itaongeza ushindani kwa mchezaji mmojammoja ndani ya timu kiujumla na endapo atapata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa basi imani yetu ni kwamba ataonyesha utofauti.

Timu zote ndani ya ligi shiriki zitacheza kwa kupambana, hili ni muhimu kuzingatia kwani mashabiki wanapenda kuona timu ikipata matokeo chanya uwanjani.

Kwa sasa ndani ya ligi tunaona timu zinashinda ugenini pia jambo ambalo lilikuwa linaonekana kuwa gumu kwa msimu uliopita ila kwa sasa mambo yamebadilika.


Mfano mzuri tunaona KMC iliweza kushinda mechi yake mbele ya Mwadui FC, pia Mtibwa Sugar iliweza kushinda mbele ya Ihefu Fc pamoja na Polisi Tanzania mbele ya Namungo.

Mbeya City wakiwa nyumbani walipoteza michezo miwili mbele ya Azam FC pamoja na Namungo FC  ambao walikuwa wageni ndani ya Uwanja wa Sokoine.

Ikiwa ligi itaendelea namna hii itafanya kila timu kutobweteka hata pale inapokuwa nyumbani lazima ikazane kusaka matokeo.Kwa kuwa wanaamini kwamba wapinzani wao wapo vizuri na dunia nzima itashuhudia wanachokifanya kupitia Azam TV.

Mechi nyingi ambazo zinaonyeshwa na Azam TV zina mvuto wa kipekee na zinaonekana kuwa tofauti jambo ambalo linapaswa pia pongezi kwa  Azam TV kwa kuamua kuwekeza nguvu kubwa kwenye soka letu.
Hii iwe ni fursa kwa wachezaji kuitumia kuuza uwezo wao nje ya nchi  kwa kuwa ligi ya Tanzania kwa sasa inafuatiliwa na wengi duniani ukizingatia kwamba mechi zote za Ligi zinarushwa mubashara ndani ya Azam TV.

SOMA NA HII  AZAM FC:HAIKUWA FUNGU LETU MTIBWA SUGAR

Ligi inaonekana kwamba imekuwa bora kwa kuwa hakuna masuala ya mcheza kwao hutunzwa kama ambavyo wengi walikuwa wakidhania na kufanyika kwa misimu kadhaa iliyopita.

Kikubwa waamuzi wawe makini katika maamuzi yao kwani Azam TV kwa sasa wanaonyesha kila kitu tofauti na awali ambapo kuna baadhi ya mechi zilikuwa hazionyeshwi.

Wanachotakiwa kukifanya waamuzi ni kufuata sheria 17 za uwanjani jambo ambalo litapunguza zile kelele na zigo la lawama pale ambapo timu inashindwa kufanya vizuri.

Sio waamuzi tu bali hata wachezaji pia wanapaswa kufuata sheria 17 za mchezo wa Soka na kuhakikisha wanacheza kwa nidhamu kubwa.

Zamani ilikuwa inaelezwa kwamba waamuzi wanakwenda na matokeo mfukoni jambo ambalo lilikuwa halipendezi na kusababisha maamuzi wakati mengine kuwa mabovu.

Viongozi na wachezaji pia wakati mwingine walikuwa wanakwenda na matokeo mfukoni ila kwa sasa mambo yamebadilika kutokana na utandawazi ambao unapelekea watu kuwa na uelewa wa mpira.

Jambo hilo halipaswi kufanyika kwa sasa ndani ya soka la Tanzania kwani hupelekea Ligi kuwa mbaya na kupoteza mvuto wa kufuatiliwa..

Kila timu imejipanga kupata matokeo chanya kwenye kila mchezo wa ligi jambo ambalo huongeza ushindani kwa kiasi kikubwa kwani hakuna timu ambayo inahitaji kupoteza mchezo wowote.

Hakuna timu ambayo inaonekana ni dhaifu mwanzo kwani wanahitaji kupata uhakika wa kuendelea kusalia ndani ya Ligi kwa kuhofia ugumu uliopo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) mpaka kuja kufanikiwa kupanda huwa ni mtihani kwao.

Zile ambazo hazipati matokeo mazuri ni wakati wa kujipanga upya  kwani ni mapema kuanza kurekebisha baadhi ya makosa ambayo yalionekana kwenye michezo iliyopita.

Baadhi ya timu hazijafanya maandalizi ya kutosha kujiandaa na msimu kutokana na muda mfupi ambao walipewa jambo ambalo lilisababishwa na janga la Corona.

Makocha wanapaswa kufanya marekebisho kwa mechi zilizochezwa mpaka sasa na kujitafakari kwa kina juu ya mwelekeo wa timu zao pamoja na mikakati yao jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kwa timu kufanya vizuri kwa michezo iliyobaki.

Ikumbukwe Ligi kwa sasa imekuwa ngumu kutokana na ushindani mkubwa uliopo na timu shiriki hivyo timu zinapaswa kuzingatia malengo waliyojiwekea.

Tunaona kwa sasa pia viwanja vingi vinafungiwa na Bodi ya Ligi Tanzania, hii ni ishara mbaya hasa baada ya ligi kuanza, kuna umuhimu wa wahusika kuwa makini katika kutunza viwanja kwani ni sehemu namba moja kwenye kutafuta ushindi.

Mpaka sasa ni viwanja vitano tayari vimefungiwa hivyo kwa kadri siku zinavyokwenda huenda vikaongezeka vingine pia.