Home Uncategorized YANGA KIGELEGELE AWAOMBA MASHABIKI KUACHA MIHEMUKO

YANGA KIGELEGELE AWAOMBA MASHABIKI KUACHA MIHEMUKO


 SHABIKI maarufu wa Yanga, Anuary Wambura ‘Yanga Kigelegele’, amewataka mashabiki wa Simba na Yanga kupunguza mihemko wanapokuwa viwanjani ili kuepuka vurugu zisizo za lazima.

 

Katika siku za hivi karibuni, kumetokea vurugu viwanjani zilizohusisha mashabiki wanaotajwa kuwa ni wa Simba na Yanga, Yanga na Coastal Union hali ambayo kila mmoja amekuwa akikemea ikiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Shabiki huyo ambaye mapema wiki hii alitembelea Ofisi za Gazeti la Spoti Xtra zilizopo katika Jengo la Global Group, Sinza Mori jijini Dar, alisema: “Mashabiki wakae wakifahamu kuwa, soka ni burudani na si uadui, wanatakiwa kuwa kitu kimoja.


“Mfano katika tukio lililotokea kwenye mechi yetu dhidi ya Mtibwa Sugar kule Morogoro, nilikuwepo uwanjani na nilishuhudia kila kitu, mashabiki wa Simba walikuwa wametoa lugha ambazo si za kiuanamichezo kwa mashabiki wa Yanga ndio maana walichukua maamuzi yale.


 “Mimi mwenyewe sipendi matukio ya ugomvi, twendeni uwanjani kwa utulivu hata kama utani utakuwepo uwe wa kawaida na kuleta furaha na si kama yale, sipendi kuona mashabiki wanakuwa maadui.

 

“Watu wanatoa lugha za kejeli wanapokuwa uwanjani ambazo zinawaumiza mashabiki wengine jambo ambalo si sahihi kwani inapelekea kuchochea hasira, hivyo tujaribu kuangalia lugha tunazotoa.


“Mashabiki wanatakiwa kupunguza mihemko na kutoa lugha ambazo hazitawakera wengine, kuzua chuki,” amesema.


Yanga Kigelele ambaye ni maarufu kwa staili yake ya kushangilia kwa kupiga vigelegele, alipokuwa Global Group, alipata muda wa kutembelea idara zote ikiwemo kitengo cha magazeti ya michezo, Spoti Xtra na Championi, Global TV Online na +255 Global Radio, kisha kufanya mahojiano maalum.

SOMA NA HII  YANGA YAPAGAWA NA POINTI MOJA ILIYOAMBULIA NDANI YA DAKIKA 180