ZUBER Katwila, Kocha Mkuu wa Klabu ya Ihefu FC amesema kuwa atatumia dirisha dogo la usajili kuboresha kikosi chake ambacho kimekuwa na mwendo wa kusuasua kwa msimu wa 2020/21 baada ya kupanda kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ikiwa imecheza jumla ya mechi 12 ambazo ni dakika 1,080 imekusanya jumla ya pointi sita na safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao matatu ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 360 huku ikifungwa jumla ya mabao 13 ikiwa na wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 83.
Katwila ameweka wazi kwamba kwenye dirisha dogo ambalo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15 atatumia nafasi hiyo kusajili wachezaji wenye uzoefu ambao watawapa matokeo mazuri.
Ikiwa nafasi ya 18 kwenye msimamo ikiwa itaendelea kubaki hapo inaweza kushuka daraja na kurejea Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa timu nne zitashuka jumlajumla na zile mbili ambazo zitashika nafasi ya 13 na 14 zitacheza playoff.
Katwila amesema:”Kikosi hakipo sawa kutokana na aina ya wachezaji ambao tupo nao wanajitahidi kupambana ila wanashindwa kupata matokeo kutokana na kushindwa kuwa na uzoefu hivyo nitatumia nafasi ya usajili wa dirisha dogo kuleta wachezaji wenye uzoefu,” .
Jana, Novemba 24, Ihefu FC iliyeyusha pointi tatu Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union.