Home Uncategorized KOCHA YANGA AHOFIA REKODI ZA TANZANIA PRISONS

KOCHA YANGA AHOFIA REKODI ZA TANZANIA PRISONS


 KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amekiri kuwa mchezo wao wa leo dhidi ya Prisons utakuwa mgumu, hasa kutokana na rekodi nzuri ya wapinzani wao wanapocheza katika uwanja wa nyumbani wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa katika mchezo wa raundi ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

 

Kaze ameliambia Spoti Xtra, kuwa ameweka mpango kazi wa kuhakikisha anaufungua ukuta wa Prisons na kupata matokeo mbele yao licha ya wapinzani wake kuwa wagumu.

 

“Kitu kizuri ni kwamba tumepata muda mzuri wa kujiandaa na mazoezi, na mazoezi ni mazuri na wachezaji wana nia ya kutafuta ushindi kwenye mechi hii na Prisons.


“Prisons wana timu nzuri, wanajua kuzuia, wana mwalimu mwenye uzoefu wa ligi lakini na sisi tumejiandaa kulingana na uzito wa mechi, hii.

 

“Hakuna timu nyingi ambazo zimewafunga wakiwa hapa hivyo tunafahamu tunatakiwa kupandisha pafomansi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,” aliweka nukta Kaze.


Meneja wa Prisons, Prosper Mtevu, alizungumzia mchezo huo akisema:-“Tunaijua vizuri Yanga, mchezo wa raundi ya kwanza baina yetu tulipata matokeo ya sare, na wanaonekana kuwa na rekodi nzuri, lakini huwezi kushinda kila siku, hivyo inawezekana kabisa sisi tukaifanya ipoteze mchezo wake wa kwanza.”


Huu unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Prisons na Yanga kwa mzunguko wa pili ambao unaanza leo kwao kusaka pointi tatu muhimu.


Mchezo wao uliopita Prisons ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United inakutana na Yanga ambayo imetoka kushinda mabao 3-0 dhidi ya Ihefu.

SOMA NA HII  HIZI HAPA DAKIKA 270 ZA MOTO KWA SIMBA KABLA YA KUINGIA MIKONONI MWA YANGA