Home Uncategorized MWIBA KWA SIMBA KESHO UWANJA WA MKAPA NI YULE ALIYEMTUNGUA MANULA

MWIBA KWA SIMBA KESHO UWANJA WA MKAPA NI YULE ALIYEMTUNGUA MANULA


KESHO Uwanja wa Mkapa, mabingwa watetezi Simba watakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Klabu ya Polisi Tanzania inayonolewa na Kocha Mkuu, Malale Hamsini.


Ndani ya Polisi Tanzania kuna wachezaji wengi ambao ni bora ndani ya uwanja katika kusaka matokeo jambo ambalo linaleta picha kwamba mchezo wa kesho hautakuwa mwepesi.


Wakati Simba wakiwa wanajivunia uwepo wa kiungo wao Ibrahim Ajibu ambaye jezi yake ni namba 10 mgongoni na kwenye ligi amefunga bao moja kati ya 29 yaliyofungwa na Simba kwa Polisi Tanzania yupo mzawa anaitwa Marcel Kaheza.

 Kaheza yeye ni mpigaji namba moja wa mipira iliyokufa ndani ya Polisi Tanzania na ni mwepesi akiwa ndani ya 18 kwenye kutoa pasi ama kufunga.


Amefunga mabao matatu na ana pasi moja ya bao. Mabao mawili amefunga kwa penalti na moja kwa mpira wa faulo aliyoijaza mazima ndani ya nyavu.

Jumla amehusika kwenye mabao manne ya timu yake ya Polisi Tanzania ambayo imefunga mabao 11 baada ya kucheza mechi13.


Hivyo Kaheza ni mtambo wa mabao ndani ya Polisi Tanzania iliyo nafasi ya sita na kibindoni ina jumla ya pointi 20.

Kesho anakutana na mabosi wake wa zamani Simba ambao Kwenye mchezo wa mwisho msimu uliopita alimtungua Aishi Manula kwa penalti.


Simba inaingia uwanjani ikiwa na presha ya kushusha gepu la pointi ambalo watani zake wa jadi Yanga wameweka kibindoni ambapo wanadaiwa pointi 11.


Yanga ipo nafasi ya kwanza bila presha ikiwa na pointi 34 na Simba ipo nafasi ya tatu na pointi zake 23 hivyo kazi itakuwa kubwa kwa timu zote mbili.


Malengo ya Polisi Tanzania ni kumaliza ligi ikiwa ndani ya tano bora huku Simba wao wanafikiria ubingwa.


Uongozi wa Polisi Tanzania, kupitia Ofisa Habari wao Frank Lukwaro amesema kuwa kila kitu kipo sawa ni suala la wakati tu.


Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa kila mchezo kwao wanahitaji pointi tatu.

SOMA NA HII  BABA: HAKUNA STRAIKA WA KUMPITA YONDANI