UONGOZI wa Mwadui FC unatajwa kufanya mazungumzo na Yanga kupata saini ya mshambuliaji wao wa zamani Ditram Nchimbi.
Nchimbi aliwahi kucheza ndani ya Mwadui FC kwa mkopo akitokea Azam FC kabla ya kuibukia Polisi Tanzania kwa sasa yupo zake ndani ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze.
Habari zinaeleza kuwa tayari uongozi wa Mwadui umetuma barua za maombi ndani ya Yanga ikihitaji kumpata Nchimbi na kama mambo yatakuwa magumu basi wameomba wapewe nyota Wazir Junior akaokoe jahazi.
Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Amri Said ambeye amechukua mikoba ya Khalid Adam ambaye alifutwa kazi kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo amesema kuwa ataboresha kikosi hicho ili kiweze kufanya vizuri kwenye mzunguko wa pili.
“Mzunguko wa pili tutafanya kazi kubwa kwa kuhakikisha kwamba tunapata matokeo mazuri ndani ya uwanja na ni jambo la msingi kwetu kuweza kupata matokeo.
“Kikubwa wachezaji ambao tutawaongeza kwenye dirisha dogo ninaamini kwamba watakuwa na msaada kwetu hivyo mipango ikakamilika kila kitu kitawekwa wazi,” .
Mwadui FC kwenye msimamo ipo nafasi ya 16 ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza jumla ya mechi 18.