FARID Mussa kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, usiku wa kuamkia leo aliwamaliza Namibia kwa kuwatungua bao moja na kusepa na tuzo ya mchezaji bora wa mchezo.
Stars imeshinda mchezo wake wa kwanza kwenye mashindano yanayohusisha wachezaji wa ndani,Chan na kuipa pointi tatu muhimu Stars.
Mchezo wa kwanza Stars ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia ambayo nayo ililazimisha sare mbele ya Guinea na kukusanya jumla ya pointi nne.
Mussa alitupia bao la ushindi dakika ya 65 na kuifanya Namibia kuyeyusha mazima pointi tatu, kituo kinachofuata ni dhidi ya Guinea, Januari 27.
Hata hivyo hakumaliza dakika zote 90 uwanjani kwa kuwa alitoka dakika ya 88 kumpisha kiungo Baraka Majogoro ambaye alikwenda kumalizia dakika zilizobaki.
Kwenye mchezo huo pia wachezaji walisimama kwa muda baada ya taa za Uwanja wa Limbe, Cameroon kuzima ghafla.
Stars inakuwa nafasi ya tatu huku Namibia ikiwa imeshaaga mashindano jumla matokeo ya mchezo wa mwisho yataamua nani atakuwa nani kwenye kundi hili D.