Home Simba SC GOMES ATOA MBINU TATU KALI SIMBA..AFUNGUKA HAYA KWA WACHEZAJI..!!

GOMES ATOA MBINU TATU KALI SIMBA..AFUNGUKA HAYA KWA WACHEZAJI..!!


KOCHA mpya wa Simba, Didier Gomes ameanza kibarua rasmi cha kuinoa timu hiyo muda mfupi baada ya kutambulishwa na baada ya kuongoza mazoezi ya kwanza juzi na jana jioni, ameanika mambo matatu anayohitaji kutoka kwa wachezaji wa timu hiyo.

Gomez (51), alitambulisha rasmi juzi na uongozi wa klabu hiyo mara baada ya kuvunja mkataba wake na El Merreikh ya Sudan na mara baada ya zoezi hilo, jioni aliungana na kikosi chake katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena huko Bunju.

Kocha huyo mara baada ya kuongoza mazoezi yake ya kwanza, aliwaambia wachezaji vipaumbele vitatu ambavyo ni lazima wavifanyie kazi vinginevyo asiyetimiza asitegemee kupata nafasi ya kucheza chini yake.

“Nimeongea na wachezaji na kuwatajia mambo kama matatu hivi ninayoyahitaji kutoka kwao. Kwanza staili ya kuwakaba wapinzani kuanzia kwenye eneo lao (pressing) ni ya muhimu sana kwangu. Mengine ni haiba nzuri na nidhamu ya hali ya juu,” alisema.

“Nidhamu ni miongoni mwa vitu vya msingi vya kufanya ufikie malengo na matarajio.Nilitaka kuongoza mazoezi. Ilikuwa ni muhimu kuwaona wachezaji ukizingatia kuna mashindano makubwa ya Simba Super Cup wiki hii na natakiwa kuiandaa timu kwa sababu ni mashindano ya Simba na tunatakiwa kuwa imara na wenye haiba nzuri.”

Gomez alisema kuwa anategemea kuona kila mchezaji wa Simba anaipigania jezi ya klabu hiyo na kuwa mfano bora nje na ndani ya uwanja kwani ndio siri ya mafanikio ya klabu yoyote.

“Wachezaji niliokuwa nao mazoezini wanatakiwa kunionyesha kile walichonacho na wanachoweza kukifanya hivyo ni vizuri. Ni fursa – muhimu kutazama ubora wao, lakini ni nafasi kwao kuonyesha kwamba wanastahili kuichezea Simba. Kwa siku za usoni ni jambo zuri hivyo natakiwa kuzoea mchakato wangu.

“Kubwa ninalolihitaji kwao ni haiba na tabia njema kwa sababu Simba ni timu kubwa unapovaa jezi unatakiwa kuwa imara akilini, hivyo hilo ni jambo ninalohitaji kwao kwenye mechi ijayo ingawa nahitaji kuwa nao wote.”

SOMA NA HII  CHIKWENDE: CHAMA, LUIS WAMENIVUTA SIMBA

Kocha huyo aliongeza kuwa: “Ligi zinatofautiana.Lakini ninachoona kwa Simba ipo katika levo za juu. Ni miongoni mwa timu 16 bora za Afrika, kwa hiyo ni timu kubwa.”

“Najua kwamba timu nyingi zinaiheshimu Simba na miongoni mwa hizo ni wapinzani wake ambao wamepangwa nayo kundi moja.”

Katika mazoezi hayo wachezaji walionekana kumfurahia kocha huyo huku kila mmoja akijitahidi kufuata maelekezo na kujua anataka nini.

Gomez ametua Simba kuchukua mikoba ya Sven Ludwig Vandenbroeck aliyechukumia mikoba kutoka kwa Patrick Aussems na makocha hao wore raia wa Ubelgiji waliiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Simba licha ya juhudi kubwa ambazo uongozi wake umekuwa ukionyesha katika kuhakikisha timu inakuwa na nidhamu, bado tatizo la utovu wa nidhamu limeonekana kuwa sugu kwa baadhi ya wachezaji jambo linalomfanya Gomez afanye kazi ya ziada kulimaliza.

Hivi karibuni kiungo wa klabu hiyo, Jonas Mkude alipewa adhabu ya faini ya Sh2 milioni baada ya kamati ya nidhamu ya klabu hiyo kumkuta na hatia ya makosa ya utovu wa nidhamu yakiwemo kuchelewa kambini.