Home Uncategorized KOMBE LA MAPINDUZI LIWE SEHEMU HALISI YA KUREJESHA UBORA KWA WACHEZAJI

KOMBE LA MAPINDUZI LIWE SEHEMU HALISI YA KUREJESHA UBORA KWA WACHEZAJI


 KAZI kubwa kwa sasa ndani ya uwanja kwa timu ambazo zimepata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi ni kusaka ushindi katika kila mechi ambazo wataingia ndani ya uwanja.

Mabigwa watetezi nao wana kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kurejea na taji lao ambalo walilitwaa msimu uliopita wa 2020.

Haitakuwa kazi nyepesi kwa Mtibwa Sugar kuweza kufikia mafanikio ambayo waliweza kufikia msimu uliopita ikiwa hawataongeza juhudi na kufanya kazi kwa kujituma.

Timu tisa ambazo zinashiriki na makundi yao matatu kila timu inaonekana kwamba ina jambo ambalo inahitaji kulifanya.

Imani yangu ni kwamba kwa namna ambavyo ushindani utakuwa mkubwa utatoa picha ya kile ambacho kipo ndani ya timu hizo.

Ikumbukwe kwamba Kombe la Mapinduzi ni sehemu ya kuonyesha uwezo kwa wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi kwenye timu zao.

Wakati huu kwa wachezaji wenye akili hutumia kuonyesha uwezo wao wote ili kulishawishi benchi la ufundi liweze kuwapa nafasi kwenye timu zao pale mashindano yatakapofika ukingoni.

Pia ni muda mzuri kwa makocha kujenga kikosi upya kwa ajili ya kurejea kwenye ubora pale watakaporejea kwenye ligi. Ipo wazi kwa sasa ligi imesimama kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi.

Na ningependa niwakumbushe wachezaji kwamba kwa wakati huu bado dirisha dogo lipo wazi wanaweza kupata sehemu ya kutokea ikiwa watapambana.

Wapo mawakala ambao hujitokeza kwenye haya mashindano makubwa na pia makocha wa timu mbalimbali wapo kwa sasa ndani ya Visiwa vya Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa mashindano haya yanarushwa duniani na kufanya iwe ni sehemu ya kutangaza vipaji vyao nje na ndani ya Zanzibar.

Nina amini kwamba wachezaji kwenye jezi zao kuna majina yao pamoja na namba zao jambo linalofungua njia kwa upande wa kujitangaza.

Wakala akikubali uwezo wa mchezaji fulani hatatakuwa na wasiwasi kuanza kumfuatilia mchezaji anayemtaka bali atakaa chini na kuanza kufuatilia rekodi za mchezaji huyo.

Ikiwa atakubali uwezo wa nyota huyo basi anaweza kufanya mazungumzo naye na kupata nafasi ya kupata changamoto mpya. Soka linaishi kutokana na rekodi nzuri uwanjani.

SOMA NA HII  Miraji avunja kanuni ya saa saba kamili?

Kwa waandaaji pia ni muhimu kuzidi kuboresha mashindano haya ili yazidi kuwa na mvuto kwa kuwa mwanzoni ilikuwa na mvuto mkubwa.

Uwepo wa timu kutoka nje ya Bongo ambazo zilikuwa zinakuja kushiriki na kuleta ushindani lilikuwa ni moja ya jambo ambalo linazidisha uzuri wa mashindano.

Ila kibaya ilikuwa ni kwamba pale wageni wanapopambana kiukweli na kusepa na kombe wakiwa ugenini hili pia nalo linapaswa litazamwe kwa wakati ujao.

Mashabiki pia ni wakati wenu wa kujitokeza ndani ya uwanja kuona burudani. Kila timu inaonekana kujipanga kusaka ushindi.

Ni wakati wa benchi la ufundi pia kutazama mapungufu na kuyafanyia kazi ili pale ligi itakapoanza kila kitu kitakuwa sawa. 

Kwa zile timu ambazo jezi zao hazina majina itapendeza ikiwa wakati ujao wataboresha hilo kwani majina na namba vinaonekana ni vitu vidogo kwa timu ila maana yake ni kubwa katika soko la biashara.