Home Uncategorized SportPesa YAMWAGA MAMILIONI KWA NAMUNGO

SportPesa YAMWAGA MAMILIONI KWA NAMUNGO


 KAMPUNI ya Michezo ya Burudani ya SportPesa imeipa udhamini wa Sh 23.3 Mil Klabu ya Namungo FC kwa ajili ya kuiwezesha timu hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wao dhidi ya Al Hilal ya nchini Sudan utakaopigwa Januari 6, mwaka huu wa marudiano.


Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Uendeshaji wa SportPesa Tarimba Abbas amesema kuwa udhamini huo walioutoa maalum kwa ajili ya mchezo dhidi ya Hilal.

Tarimba amesema kuwa fedha hizo zitaiwezesha timu hiyo kununua tiketi na matumizi mengine katika kuelekea mchezo huo mgumu ambao anaamini Namungo itapata ushindi.

“Katika kuthamini michezo SportPesa tumewapa udhamini Namungo kwa ajili ya kuwawezesha baadhi ya vitu katika kuelekea mchezo huo na kati ya hivyo ni tiketi za ndege kwa wachezaji na viongozi.

“Pesa hiyo ya Sh 23.3 Mil ni ndogo lakini tunaamini kuwa itasaidia kwa kiwango kikubwa Namungo katika kuelekea mchezo huo.

“Hatuna wasiwasi na Namungo katika kuelekea mchezo huo, tunaamini watapata matokeo mazuri na kusonga mbele katika mashindano hayo makubwa Afrika.

“Lengo la SportPesa kutoa udhamini huo Namungo ni kuona michezo inapiga hatua, hivyo SportPesa itaendelea kutoa udhamini kama ilivyokuwa kwa klabu za Simba na Yanga,” amesema Tarimba.

Akipokea hundi hiyo ya Sh 23.3Mil, Mwenyekiti wa Namungo, Hassani Zidadu amesema kuwa “Tumefarijika kwa udhamini huu ambao SportPesa imetupatia ambao kwetu ni kubwa.

“Udhamini huu utatuwezesha kununua tiketi za ndege na matumizi mengine katika kuelekea Sudan kwenda kucheza mchezo wetu dhidi ya Hilal.

“Kama unavyofahamu mchezo wa mpira wa miguu unahitaji fedha nyingi, hivyo kwa udhamini huu tunaamini kuwa utatusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuelekea mchezo huo ambao ni mgumu tunahitaji kupata ushindi ili tusonge mbele,” amesema Zidadu.

“Ningependa kutoa Rai kwa makampuni binafsi na ya michezo kujihusisha ili kusaidia timu mbalimbali za mpira wa miguu kwani michezo ni sehemu ya burudani na ndio maana mpira wa miguu ni mchezo wenye mashabiki wengi zaidi, ” aliongeza Tarimba.
SOMA NA HII  SIMBA KAZI BADO IPO LEO TAIFA MBELE YA SINGIDA UNITED