Home Simba SC PAWASA: SIMBA ILI IFANYE VIZURI KIMATAIFA IONGEZE NGUVU KWENYE KIUNGO MKABAJI

PAWASA: SIMBA ILI IFANYE VIZURI KIMATAIFA IONGEZE NGUVU KWENYE KIUNGO MKABAJI


BEKI wa zamani wa Klabu ya Simba, Boniface Pawasa amesema kuwa ili Simba iweze kutusua kimataifa ni lazima iwe na kiungo mkabaji makini ambaye atakuwa anatuliza mipira pamoja na hatari ndani ya uwanja.

Simba kwa sasa ina viungo wakabaji wawili ambao ni chaguo la kwanza kwa Kocha Mkuu, Didier Gomes, Mzamiru Yassin na Thadeo Lwanga huku Jonas Mkude na Said Ndemla wakiwa bado hawajapata nafasi kwenye kikosi chake.

Leo kikosi kinatarajia kukwea pipa kuelekea Congo majira ya saa 10:00 jioni ambapo kina mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi dhidi ya AS Vita unaotarajiwa kuchezwa Februari 12.

Pawasa ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ya Ufukweni, amesema kuwa kila kitu kinawezekana ikiwa watakuwa na kiungo mkabaji makini.

“Kwenye mechi za kimataifa ni muhimu kuwa na kiungo mkabaji mwenye nguvu na uwezo wa kukaa na mpira muda mwingi jambo litakalopunguza mashambulizi kwa upande wao.

“Kwa namna ambavyo nimeona kikosi cha Simba kikiwa na Lwanga bado kuna kitu kinahitajika kwa upande wa kiungo mkabaji kwa kuwa ulimwengu wa mpira umebadilika.

“Nimemuona Lwanga naona bado anajitahidi ila hajawa kwenye ule ubora wake ambao ninaujua. Ninawajua wachezaji wanaotoka Uganda ni watu wa nguvu sana hivyo ni suala la kusubiri na kuona namna gani inaweza kuwa,” amesema.

SOMA NA HII  CLATOUS CHAMA AWEKA REKODI YAKE BONGO