Home news MAELFU WAJITOKEZA KUMUAGA MAGUFULI, LEO ZOEZI LINAENDELEA, WANAMICHEZO, WASANII PIA

MAELFU WAJITOKEZA KUMUAGA MAGUFULI, LEO ZOEZI LINAENDELEA, WANAMICHEZO, WASANII PIA


 RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, jana Machi 20 aliongoza maelfu ya Watanzania kuaga mwili wa Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli.

Kuaga kwa mwili wa Magufuli ambaye alitangulia mbele za haki Machi 17 kutokana na matatizo ya moyo kwa mujibu wa Samia kunaendelea leo pia Machi 21 kwa wakazi wa Dar es Salaam ambapo jana ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi na ilianza ibada baada ya mwili kutolewa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.

Kwenye ibada iliyofanyika kanisa la Mtakatifu Peter ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na waumini ambapo baada ya ibada msafara ulipita katika maeneo ya Morocco, Kinondoni, Magomeni, Kigogo, Ilala Boma, Keko, Duce, Uwanja wa Mkapa na uliagwa na viongozi Uwanja wa Uhuru.

Katika njia zote hizo Wananchi wengi walijitokeza wakiwa wanatupa maua barabarani. Kutandika khanga ikiwa ni ishara ya kuomboleza huku wengine wakionekana kutokwa na machozi wakimlilia Magufuli.

Pia ratiba ilifanyiwa mabadiliko kidogo ambapo leo Machi 21 wananchi wa Dar es Salaam wataaga mwili na utasafirishwa kwenda Dodoma ambao wataaga mwili Machi 22 kisha utasafirishwa kwenda Visiwani Zanzibar, Machi 23.

Machi 24 Wananchi wa Mwanza wataaga mwili na Machi 25 Wanafamilia na Wananchi wa Chato wataaga mwili na Machi 26 shughuli za mazishi kufanyika Chato baada ya ibada mkoani Geita.


Wanasiasa, wasanii, viongozi wa dini pamoja na wanamichezo walijitokeza kwa wingi, Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kushiriki ibada ya maombolezo.

Miongoni mwa waliokuwepo ni pamoja Askofu Mkuu Mstaafu, Policarp Pengo, Mrisho Mpoto, Nassib Abdul, ‘Diamond’, Hamonize, Mohamed Dewji, ‘Mo’. Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Thaddeus Ruwai’chi, Mama Nyeyere, Anna Makinda.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.

Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume,Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bache.

Leo ni zamu ya wakazi wa Dar na mikoa ya karibu ambao wamejitokeza kwa wingi, Uwanja wa Uhuru kutoa heshima za mwisho.

SOMA NA HII  DAKIKA CHACHE KABLA YANGA HAWAJASHUKA DIMBANI..HIZI HAPA SIKU 313 ZA NABI NA PANDA SHUKA YAKE...