Home Azam FC AZIZ KI AFUNGA MWAKA KWA AINA YAKE…. AZAM NAO WASEPA NA REKODI...

AZIZ KI AFUNGA MWAKA KWA AINA YAKE…. AZAM NAO WASEPA NA REKODI HII

Habari za Yanga

Wamefunga mwaka kibabe! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiungo mshambuliaji nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI na timu nzima ya Azam FC, kufunga mwaka kibabe katika Ligi Kuu Bara inayosimama kwa muda kupisha msichuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Afcon zitakazopigwa Ivory Coast.

Aziz KI, alifunga bao pekee wakati Yanga ikiizamisha Tabora United kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kufikisha mabao 10 kupitia mechi 11 kwa msimu huu akivunja rekodi binafsi aliyoiweka msimu uliopita alipomaliza na mabao tisa kupitia mechi 30, lakini Azam FC ikiuaga mwaka 2023 ikiwa kileleni mwa msimamo ikivuna pointi 31 katika mechi 13.

Aziz Ki anaonekana kuwa kwenye kiwango bora zaidi tangu ajiunge na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ikumbukwe nyota huyo pia alipika bao moja kwenye ushindi wa kwanza wa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga ilipoizima Medeama ya Ghana kwa mabao 3-0.

Wakati Yanga ikimaliza vizuri mwaka huku ikiwa na michezo miwili mkononi, mtani wao Simba alivutwa shati dhidi ya KMC kwa kutoka sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.

Wenye uwanja huo, Azam FC walikuwa wakiwachora tu kwani walitoka kufanya maangamizi, Bukoba kwa kuwashushia mvua ya mabao 4-0 Kagera Sugar kiasi cha hadi kocha wa kikosi hicho, Mecky Maxime kufungashiwa virago vyake.

Nini kimetokea katika michezo ya raundi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kupisha maandalizi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ambayo inajiandaa na fainali za mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februar1 11, 2024.

AZAM BABA LAO

Vijana wa Youssouph Dabo ndio timu ambayo imeumaliza mwaka kibabe kwa kuongoza msimamo licha ya kuwa mbele kwa michezo miwili lakini pili kwa kutoa kipigo kikubwa zaidi kwenye raundi ya mwisho kabla ya ligi kusimama.

Ushindi wa mabao 4-0 ambao Azam FC iliupata dhidi ya Kagera Sugar umeifanya kuwa timu iliyoibuka na ushindi mnono zaidi huku wakifuatiwa na Mtibwa Sugar ambayo imetoka kuifunga Mashujaa kwa mabao 2-1.

Dabo ambaye alikuwa kwenye presha baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo kwenye ligi mwishoni mwa Oktoba, alisema anavutiwa na uwajibikaji wa wachezaji wake kwa sasa lakini ni wazi kuwa wanatakiwa kuwa bora zaidi ili kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata ya ligi.

Kabla ya kuifunga Kagera Sugar, Azam ilizifunga JKT Tanzania kwa mabao 2-1 huku balaa likiwakuta KMC na Mtibwa Sugar ambao kila mmoja alitandikwa mvua ya mabao 5-0.

“Kushinda ni jambo zuri kwa sababu hata kwa upande wa wachezaji huongeza hali ya kujiamini, tupo kwenye mwelekeo mzuri na ninafuraha na hilo, tunatakiwa kuendelea kujitoa bila ya kubweteka na matokeo huku tukiboresha udhaifu wetu ambao umekuwa ukijitokeza,” anasema kocha huyo na kuongeza;

“Binafsi nataka kuona tukipata mafanikio makubwa, sio tu kwenye ligi ya ndani hadi Afrika lakini ili tufanikishe hilo tunatakiwa kwenda hatua kwa hatua.”

VITA YA UFUNGAJI

Kufunga kwa Aziz Ki, Waziri Junior, Jean Baleke na Feisal Salum kwenye raundi za mwisho kwa mwaka huu kumekoleza vita ya ufungaji bora ambayo inaweza kuendelea kupamba moto zaidi mwakani baada ya kumalizika kwa Afcon pamoja na Kombe la Mapinduzi.

Aziz ambaye alifunga bao pekee ambalo liliipa ushindi Yanga dhidi ya Tabora United amefikisha mabao 10 na ndiye kinara wa kufumania nyavu, Feisal naye alitupia moja dhidi ya Kagera amefikisha mabao manane sawa na Baleke aliyefunga bao la pili la Simba dhidi ya KMC.

Waziri naye yumo kwenye vita hiyo, mabao mawili aliyofunga dhidi ya Simba, yamemfanya kufikisha mabao saba sawa na Maxi Mpia Nzengeli wa Yanga.

Akiongelea siri ya mabao yake mawili aliyofunga dhidi ya Simba, Waziri anasema, “Mabeki wa Simba ni wazuri, kufunga mabao mawili nilizingatia sana alichonisisitiza kocha kwamba nisihofie chochote kazi yangu iwe kukimbia nyuma ya mabeki kuangalia makosa watakayofanya niyafanyie kazi. Siyo mara ya kwanza kuifunga Simba, nimeifunga Mwanza nikiwa na Mbao, nikiwa na Toto Africa, nimeifunga kwa Mkapa na leo hapa Azam Complex.”

NNE BORA

Ni Azam na Yanga ambazo zimekuwa zikipishana kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Bara japo kuna kipindi mwanzoni mwa msimu Simba iliongoza, vita kubwa kwa sasa mbali na kuwania usukani wa ligi hiyo ipo kwenye nafasi nne za juu ambapo KMC, Singida BS, Coastal Union na Dodoma Jiji zinapigania.

Sare ambayo KMC imeipata dhidi ya Simba imeifanya kumaliza mwaka ikiwa nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 21 ikiwa nyuma kwa pointi mbili tu ambazo imeachwa na Simba ambayo ipo kwenye nafasi ya tatu. Simba ipo nyuma kwa michezo minne ukilinganisha na KMC.

Kufungwa kwa Singida BS yenye pointi 20 dhidi ya Geita Gold hata hivyo kuliifanya KMC kutokuwa na presha kubwa ya matokeo hivyo kupata kwao pointi moja dhidi ya Simba kulitosha kuwatenganisha na wapinzani wao hao kwenye nafasi ya nne.

Coastal yenye pointi 19 na Dodoma Jiji yenye pointi 18 zina nafasi ya kupigania kumaliza katika nne bora wakati ambapo mikiki ya ligi itarejea.

VIBARUA KUOTA NYASI

Maxime amekuwa kocha wa tisa kufungashiwa virago vyake kwenye ligi msimu huu, hatua hiyo Kagera Sugar iliifikia kufuatia matokeo mabaya ya timu hiyo ambayo ilikumbana nayo ikiwemo kufungwa mechi tatu mfululizo ambazo ni dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwa mabao 1-0 Simba (3-0) na Azam FC (4-0).

Makocha wengine wa Ligi Kuu Bara ambao vibarua vyao viliota nyasi ni Zuberi Katwila (Ihefu), Denis Kitambi (Namungo), Hemed Suleiman ‘Morocco’ (Geita Gold), Robertinho (Simba), Felix Minziro (Prisons), Habibu Kondo (Mtibwa), Abdallah Mohamed ‘Baresi’ (Mashujaa) na Mwinyi Zahera (Coastal).

VITA MKIANI

Ihefu, Kagera Sugar, Mashujaa na Mtibwa Sugar ndio timu ambazo zimemaliza vibaya mwaka kwa kuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Licha ya kuwa Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi kwenye mchezo wake wa mwisho wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa bado ina kazi ya kufanya kujinasua kwenye nafasi ya mwisho ambayo wanaburuza wakiwa na pointi nane.

Mashujaa ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi tisa huku Kagera na Ihefu zikiwa kwenye nafasi ya 14 na 13 wakiwa na pointi 13 kila mmoja.

SOMA NA HII  MWENYEKITI WA SIMBA SC AFARIKI DUNIA