Home Simba SC NIDHAMU INAHITAJIKA KWA SIMBA KUIKABILI KAIZER CHIEFS KWA MKAPA

NIDHAMU INAHITAJIKA KWA SIMBA KUIKABILI KAIZER CHIEFS KWA MKAPA


 WAWAKILISHI wetu wa Tanzania kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wameanza kwa kuchechemea katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya robo fainali dhidi ya Kaizer Chiefs.


Shirikisho la Soka la Afrika, (Caf) linashangaa namna ambavyo Simba imeweza kufungwa mabao yote yale manne huku mengi yakiwa ni ya aina moja kwa kuwa ilikuwa na rekodi bora hatua ya makundi.


Nadhani wengi wanaweza kuhoji namna gani Caf wameshangaa Simba kufungwa mabao hayo manne ni kupitia ile video yao ambayo waliipandisha kwenye ukurasa wao wa Istagram.


Katika hali ya kawaida ukiitazama ile video lazima ukasirike hasa ukiwa ni Mtanzania ambaye unapenda kuona taifa la Tanzania likisonga mbele katika maisha ya soka.


Ipo wazi mabao ambayo wamefungwa Simba inaonesha kwamba hawajawa imara kwenye mipira ya juu jambo ambalo linawapa shida katika kulinda lango ambalo lilikuwa linalindwa na Aishi Manula.


Kupitia mabao hayo manne ni darasa kwa Simba kwamba inapaswa kujilinda na kutambua kwamba wachezaji ambao wanacheza nao ni imara kwa mipira ile ya juu pamoja na matumizi mazuri ya mipira iliyokufa.


Hatua ya mtoano ni fainali jambo ambalo ambalo wapinzani waligundua na kuwaacha Simba wacheze mpira huku wao hesabu zao zikiwa ni kupata matokeo kwa namna yoyote.


Wamekuwa imara kwenye mipira ya kona pamoja na kuifikia mipira ya juu kwa namna yoyote ile walikuwa wanapambana hivyo  lazima Simba ianze kupiga hesabu upya na kubadili mbinu.


Kazi kubwa kuelekea kwenye mchezo wa marudio ambao unatarajiwa kuchezwa leo Mei 22 inapaswa ianze kwa kila mchezaji mpaka benchi la ufundi kuanza na nidhamu kwa wachezaji wa Kazier Chiefs kisha kila mmoja akatimiza jukumu lake.


Inawezekana kwamba Simba ilikuwa na nafasi ya kushinda ama kulazimisha sare ila mfumo na namna ambavyo wachezaji waliwachukulia wapinzani wao kawaida huenda kiliwagharimu.


Suala la kutazama msimamo wao na kulinganisha nafasi yao na hapa Tanzania ninadhani liliwachanganya Simba na kuamini kwamba wanawamudu Kaizer Chiefs kirahisi kwa kuwa ipo nafasi za chini.


Kwa matokeo ambayo wameyapata nina amini kwamba benchi la ufundi kuna jambo wamegundua na litafanyiwa kazi kwa wakati ujao kwa hesabu kali ambazo zitawapatia matokeo.


Kikubwa ambacho kinahitajika ni kuwa na mipango bora na nidhamu kwa mpinzani kwa ajili ya kupata matokeo kwenye mchezo ujao.


Muda wa kujipanga upo na kupata matokeo chanya inawezekana kwa njia moja ya kukubali kwamba mlikosea na sasa mnakwenda kujipanga upya kwa ajili ya kushinda mchezo ujao mbele ya Kaizer Chiefs.

SOMA NA HII  BAADA YA KUWATIKISA WAMOROCCO CAF....SIMBA SC KUJA NA MPANGO HUU KABAMBE WA KUTOBOA....


Ipo wazi kwamba tayari mbinu zenu za ushindi zipo mikononi mwa Kaizer Chiefs jambo ambalo linawezekana kwa kila timu ambayo itajipanga vizuri.


Kila mmoja anahitaji ushindi na ni wakati huu wa kujua nani ambaye atakuwa mshindi katika mchezo wa mwisho ambao utakuwa na ushindani mkubwa na kila kitu kinawezekana.


Dua za Watanzania zipo pamoja na Simba kwa kuwa wawakilishi wetu Namungo kwenye Kombe la Shirikisho tayari wameshaondolewa hatua ya makundi.


Ni Simba pekee kwa sasa wamebaki kuiwakilisha Tanzania kimataifa na imani yangu ni kwamba bado wana nafasi ya kufanya vizuri.


Zile dakika 90 za mwanzo zimekwisha na ushindi kuwa mikononi mwa Kaizer Chiefs zimebaki dakika 90 za maamuzi ambazo zitatoa mshindi wa jumla ambaye atatinga hatua ya nusu fainali.


Kila la kheri kwenu na imani yetu ni kwamba kila mmoja atakuwa anahitaji ushindi na wachezai wamepewa maelekezo ya kufanya hivyo jukumu lao ni kujituma na kufanya kazi kwa juhudi.


Jambo la msingi kwa wachezaji ni kuzingatia kwamba nidhamu ni muhimu katika kutafuta matokeo kuelekea kwenye mchezo wa maamuzi ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika.


Ukiachana na suala la Simba kusaka matokeo katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuna timu ambazo zinapambana kushuka daraja na nyingine tayari zimepanda daraja.


Tayari Mbeya Kwanza na Geita zina uhakika msimu ujao kuwa ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kupambana kufikia malengo ambayo walikuwa wamjiwekea.


Zile ambazo zimeshuka kazi yao sasa ni kujipanga kwa ajili ya msimu ujao kusaka ushindi katika mechi zao ambazo zinakuja na imani yangu ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa.


Kila la kheri kwa timu ambazo zimepanda na nina amini kwamba zitafanya vizuri kuendeleza ule ushindani ambao zilikuwa zinaonyesha ndani ya Ligi Daraja la Kwanza.


Kazi kubwa kwa wachezaji iwe kutafuta ushindi katika mechi zote ambazo watacheza na kupambana kwa hali na mali kupata wanachostahili.


 Mbeya Kwanza na Geita hapo kazi inaanza kwani kila jambo linapoisha kuna mwanzo mwingine tena. Huku kazi ni moja kusaka pointi tatu kwenye kila mechi.


Mwendo uwe uleule wa kupambana bila kuchoka katika kusaka ushindi ndani ya uwanja na inawezekana. Kila la kheri.