UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa utawafuata wapinzani wao JKT Tanzania kwa tahadhari kubwa huku wakihitaji ushindi kupata pointi tatu muhimu.
Mei 15, Uwanja wa Majaliwa ubao ukisoma Namungo FC 0-0 Yanga uliwafanya mashabiki na wachezaji kupoteza furaha kwa sababu walifutiwa bao lao jambo lilofungwa na Yacouba Songne baada ya mwamuzi kulikataa bao hilo jambo lililowafanya wagawane pointi mojamoja.
Leo Mei 17 kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuanza safari kuelekea Dodoma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania unaotarajiwa kuchezwa Mei 19, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro amesema kuwa wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
“Tunawafuata wapinzani wetu JKT Tanzania, Dodoma kwa tahadhari kubwa na tunatambua kwamba ni timu imara hivyo nasi lazima tuwaheshimu.
“Imani yetu ni kwamba tutapata pointi tatu kwa kuwa kila mchezo kwetu ni muhimu kushinda ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea,”.
Kwenye msimamo wa ligi, Yanga ipo nafasi ya pili na pointi 58 baada ya kucheza mechi 28 inakutana na JKT Tanzania iliyo nafasi ya 12 na pointi 33.