Home Simba SC GOMES AAGIZA ‘BEKI LA DUNIA’ KUSAJILIWA SIMBA..

GOMES AAGIZA ‘BEKI LA DUNIA’ KUSAJILIWA SIMBA..


LIGI Kuu Bara imesaliwa raundi nne tu kabla haijamalizika msimu huu, huku ukuta wa Simba ukionekana ndio imara zaidi kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao hadi sasa, lakini kama unadhani hilo limefanya Kocha Didier Gomes abweteke basi pole yako, kwani Mfaransa huyo sasa ni kama anataka sifa!

Inaelezwa, kocha huyo amewaangalia mabeki wake wa kati waliopo kwa sasa kikosini, akiwamo Pascal Wawa, Joash Onyango, Erasto Nyoni, Kennedy Juma na Ame Ibrahim, lakini anawaambia mabosi wake, bado anataka kitasa kingine kipya chenye makali zaidi ya mabeki alionao.

Taarifa  kutoka ndani ya Simba kuelekea katika usajili huo ikisema beki wao wa kati Pascal Wawa amewapasua kichwa kutokana na kiwango chake ambacho ameonyesha pamoja na mahitaji ya timu msimu ujao.

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa Simba wanatafuta beki wa kati mwenye uwezo zaidi ya Wawa, katika kuokoa mipira ya chini na juu, kuanzisha mashambulizi, utulivu anapokuwa na mpira pamoja na kuwazuia washambuliaji wasumbufu kama Jean-Marc Makusu anayetajwa kutakiwa na Yanga.

“Kocha kati ya maeneo ambayo anahitaji usajili ufanyike tena kwa mchezaji aliyekuwa timamu na ukamilifu ni beki wa kati ambaye atakuja kuongeza nguvu na uimara wa safu yetu ya ulinzi katika mashindano ya kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongezea;

“Kocha hataki beki mwenye uwezo wa kuzuia tu bali anataka ambaye tukiwa na mpira anaweza kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi ndefu na fupi kama ambavyo Wawa huwa anafanya katika michezo mbalimbali.

“Kocha ametuambia kama tutakosa beki wa namna hiyo wala tusifikirie jambo lolote la mabadiliko katika eneo hilo, lakini kama tutampata tumpelekee jina lake na atamuangalia kama ataridhika naye hapo ndio atatoa uamuzi wa huyo mpya au atabaki na ambao tunao wakati huu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Hivyo tupo katika kibarua cha kutafuta beki mwenye sifa kama za Wawa, lakini awe na uwezo zaidi yake kama tukishindwa kumpata maana yake hakutakuwa na mabadiliko lakini kama tutampata sahihi kulingana na kocha wetu ambavyo anahitaji maana yake tutamsajili.”

SOMA NA HII  VITA VIPYA NDANI YA SIIMBA...BALEKE VS PHIRI HAPATOSHI

Simba kama watampata mchezaji wa kigeni ambaye anacheza kwenye eneo hilo la beki wa kati au mahala kwingine kokote maana yake watalazimika kumuacha mchezaji mmoja wa kigeni walionao wakati huu kwani wapo kumi na kanuni inataka idadi hiyo.

Miongoni mwa nyota wa kigeni wanaotajwa huenda wakaachwa au kutolewa kwa mkopo ni winga Perfect Chikwende aliyeshindwa kuonyesha makali yake kwa nusu msimu aliokuwa katika kikosi cha Simba, akitokea FC Platinum ya kwao Zimbabwe.