Home FA Cup SIMBA SC YAIZIDI KETE AZAM FC

SIMBA SC YAIZIDI KETE AZAM FC


MCHEZO wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Azam FC kesho huko Songea, umeshikilia hatma ya Simba kuweka rekodi ya kubeba mataji matatu kwa mpigo ndani ya misimu miwili mfululizo.

Ubora wa timu hizo katika mechi za hivi karibuni zinaufanya mchezo huo kuwa mgumu, lakini rekodi mbili zinaibeba Simba dhidi ya wenzao kisaikolojia kuelekea katika mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Majimaji, Songea.

Rekodi hizo ni ile ya matokeo bora katika mechi za karibuni za mtoano za michuano tofauti ikiwamo ligi, pia kwa mechi ambazo kila timu imecheza Uwanja wa Majimaji.

Katika mechi tano zilizopita zilizozikutanisha timu hizo katika mashindano tofauti na Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara tatu huku Azam ikishinda mara mbili tu.

Aprili 29, 2017, Simba iliichapa Azam bao 1-0 katika nusu fainali ya ASFC, lakini Julai 13, 2018, Azam walilipa kisasi kwa kuichapa Simba mabao 2-1 katika fainali ya Kombe la Kagame.

Mwaka uliofuata, Azam ikaichapa Simba 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na baada ya hapo ikawa na unyonge kwa mechi mbili zilizofuata.

Agosti 17, 2020, Simba iliichapa Azam mabao 4-2 katika Ngao ya Jamii 2020 kisha kuicharaza tena 2-0 katika nusu fainali ya ASFC.

Ukiondoa hilo, Simba pia imekuwa ikipata matokeo mazuri pindi inapocheza katika Uwanja wa Majimaji kulinganisha na Azam FC.

Katika mechi tano zilizopita Simba ikicheza Majimaji, imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare mbili, ikifunga mabao nane na kufungwa mbili, wakati Azam imepata ushindi mara mbili na kutoka sare tatu, imefumania nyavu mara sita na kufungwa nne.

Beki wa Simba, Erasto Nyoni alisema kuwa mchezo huo dhidi ya Azam FC utakuwa ni wa kipekee kwa timu yake na yeye mwenyewe na watahakikisha wanaibuka na ushindi

“Ni mechi ambayo narudi nyumbani Songea baada ya muda mrefu hivyo ni jambo la kufurahisha. Tunafahamu mechi itakuwa ngumu. Azam ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri lakini kwa upande wetu tumejipanga tuweze kupata ushindi hivyo tunawaomba mashabiki wetu na wakazi wa Songea wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono,” alisema Nyoni.

SOMA NA HII  YANGA YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO, KUISUBIRI SIMBA V AZAM FAINALI