Home Simba SC STRAIKER MPYA SIMBA SC HUYU HAPA…

STRAIKER MPYA SIMBA SC HUYU HAPA…

 


MASTAA wa zamani wa Simba, wametoa sifa za straika mpya wanayetaka kumuona msimu ujao kwenye kikosi hicho. Wamesisitiza kwamba kama viongozi wakisajili mchezaji huyo Simba msimu ujao itatinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Beki na nahodha wa zamani wa Simba, Boniface Pawassa na Zamoyoni Mogella wamesisitiza kwamba usajili mpya wa Didier Gomes unahitaji straika mwenye uwezo mkubwa wa kutupia kwa kichwa kama walivyofanya Kaizer Chief kwenye robofainali ya Afrika.Mogella alisema; “Simba wanahitaji sana mtu wa kufunga mipira ya juu zaidi kuliko hao waliopo na ndio maana wakakosa kutinga hatua ya nusu fainali, ila kwa sasa hapa Tanzania ushindani wa timu dhidi ya Simba bado mdogo, upo timu za juu Afrika.”

Gwiji huyo alisema kwamba Simba wana mipango mingi ya maana lakini wanapaswa kutuliza kichwa kupanga mashambulizi yao upya haswa kwenye usajili kuhakikisha wanapata straika wa aina hiyo ili watembee kifua mbele zaidi.

Alisema kwamba kwa ligi ya ndani Simba haipati upinzani mkubwa hivyo wanapaswa kuelekeza usajili wao kwenye michuano mikubwa ya Afrika msimu ujao. Naye Ezekiel Kamwaga ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani Simba alisema; “Mechi ya robo fainali Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ilituonyesha tulipo tunahitaji mlinzi wa kati mwenye uwezo wa kucheza mipira ya juu.

“Ukitazama timu kunatakiwa pia mfungaji, pia kulia aongezwe mtu, yupo Duchu lakini akiumia Kapombe ni kazi sana japokuwa yupo Erasto ila kunahitajika mtu mwingine,” alisema Kamwaga.

Alisema Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu wanahitaji mwenzao ambaye atakuwa anatembea zaidi, akimtolea mfano Charles Ilamfya ambaye alitolewa kwa mkopo baada ya kuonekana hana ushindani na aliowakuta akisisitiza anahitajika mtu mwenye kasi kama Okwi wakati ule.

Pawassa naye alisema ulazima wa kusajili upo mkubwa kwenye safu ya mlinzi wa kati, kiungo namba nane ambaye atapeleka mashambulizi kwa haraka.

“Sawa Simba ina viungo wengi lakini anahitaji mwenye kasi ya haraka kwenye eneo la hatari wanamuhitaji maestro, pia mshambuliaji zaidi kuwafanya wenzake waweze kupambana sababu Bocco anapanda na kushuka,” alisisitiza.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA MASTAA SIMBA WALIVYO....MBRAZILI AANZA NA MIKWARA...AWAPA 'MAKAVU LIVE'..

Alisema, pia anatakiwa kupatikana beki mzoefu mwenye uwezo wa kucheza namba ya kulia na pia ya kushoto kwa sababu Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe wanatakiwa wapate mtu wa kuwapa changamoto itakayowafanya wazidi kuwa bora zaidi.

Kocha wa Simba, Didier Gomes akizungumza na gazeti la Mwanaspoti juzi alisisitiza kwamba anacho anachokifikiria kichwani na atakitoa baada ya kumalizika kwa msimu huu.

“Usajili wa wachezaji wa ndani nadhani siuhitaji mkubwa kwetu kwani ambao nipo nao katika timu ni bora mno na nimewaeleza nahitaji kuwa nao zaidi lakini kama kuna ambaye atapata maslahi mengine anaweza kwenda nampa ruhusa na nafasi yake tutaongeza.

“Wachezaji wa nje ya nchi, ndio tutasajili kwani kuna hitaji hilo, lakini tuliache kwanza hili muda ukifika nitalieleza kwa upana kwani sasa akili ni kuchukua ubingwa wa ligi pamoja na kombe na Shirikisho (ASFC),” alisema Kocha huyo ambaye amepania kusuka Simba mpya inayocheza soka lake.

Gazeti la Mwanaspoti linafahamu Gomes, miongoni mwa wachezaji ambao anavutiwa nao ni Edward Manyama ambaye Simba imemsajili kwa usiri mkataba wa miaka mitatu na Kibu Denis ambaye pia ana dili la kwenda TP Mazembe.

Gomes alisema kwa ambavyo anafuatilia mashindano ya ndani pamoja na uelewa aliokuwa nao katika ligi mbalimbali pamoja na mashindano ya kimataifa Simba watafanya usajili mzuri na wa kiwango cha juu akili yao ikiwa kushindana zaidi kimataifa msimu ujao.