Home Yanga SC BAADA YA KUICHAPA SIMBA, SENZO AWAPIGA MKWARA WACHEZAJI YANGA

BAADA YA KUICHAPA SIMBA, SENZO AWAPIGA MKWARA WACHEZAJI YANGA


KIKOSI cha Yanga kimerudi kazini jana baada ya mapumziko matamu ya ushindi dhidi ya watani wao Simba wikiendi iliyopita lakini wakifika tu watakutana na ujumbe huu.

Afisa Mshauri wa mambo ya uongozi wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa amenukuliwa na Mwanaspoti timu yao ilipigana vita ngumu kupata ushindi huo wa bao 1-0 mbele ya Simba.

Alisema baada ya furaha ya ushindi huo kitu cha kwanza watakachowaambia wachezaji wao ni kusahau haraka ushindi huo na kurejea kazini na akili mpya ya mapambano mengine katika mechi zao tatu za kufungia msimu.

Bosi huyo alisema timu yao inatakiwa kushinda vizuri mechi zao mbili za ligi dhidi ya Ihefu na ile ya kufunga pazia ugenini dhidi ya Dodoma Jiji.

“Wachezaji na makocha walifanya kazi nzuri, walipambana katika vita ngumu, ushindi ule una maana kubwa kwetu na mashabiki wetu.

“Furaha inatakiwa ifikie tamati na mambo mengine yaendelee, tunatakiwa kushinda mechi hizi mbili za ligi zilizobaki na tushinde vizuri katika kumalizia ligi,” alisema na kuongeza,

“Simba hawatakuja kirahisi tena mchezo ujao utakuwa mgumu mara tatu wa huu uliopita, hutakiwi kuingia katika mechi ya namna hiyo na kumbukumbu za kushinda mechi iliyopita, tunatakiwa kufuta na kusahau kama tulishinda kila mmoja kuanzia shabiki, mwanachama, sisi viongozi makocha na wachezaji wote tunatakiwa kuwa na mkakati na mpango mzuri.

“Nafurahi sasa kuona kuna umoja mkubwa ndani ya klabu hii, sasa naona nguvu ya wananchi tangu tumetoka katika mkutano wa mabadiliko kila mmoja anamsikiliza mwenzake kwa umoja, hii ndio hali halisi inayotakiwa.”

SOMA NA HII  PASI ZA YAO KUAMUA MATOKEO YA YANGA DABI YA KARIAKOO