Home Yanga SC NABI AIHOFIA SIMBA FAINALI SHIRIKISHO

NABI AIHOFIA SIMBA FAINALI SHIRIKISHO


KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa licha ya kustahili shangwe la kumfunga mtani wao Simba kwenye mchezo wao wa Jumamosi, lakini wanapaswa kuwa makini katika maandalizi yao kuelekea mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho, kwani anaamini Simba watakuja katika mchezo huo wakiwa na hasira zaidi.

Yanga juzi Jumamosi iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa katika dimba la Mkapa Dar es Salaam, ambapo ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 70 baada ya kucheza michezo 32 na kuzidi kujiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa juzi wa kiporo, Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana tena katika mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho la Julai 25, mwaka huu.

Akizungumzia mchezo huo wa fainali, kocha Nabi amesema: “Tunashukuru kwa ushindi ambao tumeupata dhidi ya Simba, nikiri wazi kuwa tulicheza dhidi ya timu nzuri na inayoundwa na wachezaji wengi bora, ushindi huu unatupa nafasi ya kusheherekea lakini hatupaswi kujisahau kwani tunakwenda kukutana nao katika mchezo mwingine wa kombe la Shirikisho.

“Najua watakuja wakiwa na hasira zaidi kuelekea mchezo huo, ili kutaka kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Jumamosi, hivyo tunapaswa kujipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu miwili iliyosalia na kujipanga mapema kwa ajili ya mchezo wa fainali Julai 25.”

SOMA NA HII  MASHINE MPYA YA YANGA KAMILI GADO KUANZA KAZI