Home Makala NAWAKUMBUSHA WAAMUZI, YANGA V SIMBA, KIGOMA

NAWAKUMBUSHA WAAMUZI, YANGA V SIMBA, KIGOMA


 WAKATI umewadia na muda umebaki
 mchache sana kabla ya watani wa jadi kuvaana kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Historia inakwenda kuandikwa kwa uwanja huo kuwakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba katika mechi muhimu ya fainali ya Kombe la Shirikisho.

Fainali ambayo imo katika rekodi ya kuwakutanisha watani wa jadi kucheza mechi mbili ndani ya mwezi mmoja na hapo hakuna mechi ya kirafiki.

Mwezi huu wa Julai, tayari Yanga wamemfunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo iliihakikishia Yanga kusimama katika nafasi ya pili ya ligi hiyo lakini ikaizuia Simba kuchukua ubingwa mapema, mikononi mwa watani wake Yanga.

Hii ni mechi ya pili, mechi ambayo Yanga wanalitaka Kombe la shirikisho, wanataka kumvua Simba ubingwa na kuthibitisha ushindi wao katika mechi iliyopita wala haukuwa wa kubahatisha.

Kwa upande wa Simba, wanataka kutetea ubingwa wao, wanataka kulipa kisasi na tatu kuonyesha Yanga waliwaotea katika mchezo ule ambao wengi hawakutarajia kuona Simba wanapoteza.

Wakati hayo yanakwenda kutokea na matokeo tukisubiri dakika 90 za mchezo huo, niwakumbushe waamuzi kwamba mwamuzi wa mchezo uliopita Emmanuel Mwanembwa alileta shida kubwa ambayo imeacha malalamiko.

Shida hiyo ilikuwa wazi na ilionekana ni kama mwamuzi alipanga kumaliza mchezo huo bila ya kutoa penalti au kutoa kadi nyekundu hata kama ilitakiwa.

Tuliona rafu kadhaa ambazo wakati mwingine tungeweza kusema zilistahili kadi nyekundu kabisa. Lakini mwamuzi hakutoa hata kadi ya njano ikionekana wazi alipania kuubalansi mchezo.

Kulikuwa na penalti, kila mmoja aliona lakini mwamuzi hakutoa pigo la penalti na hii ni ile sehemu ya kuonyesha kwamba kunakuwa na mwenendo au mwelekeo wa kisiasa unaotokana na ukubwa wa mechi ya Yanga na Simba, waamuzi hawapaswi kuingia huku.

Kama ni kadi, basi mtu ale kadi na kama ni penalti basi mara moja itolewe kwa mujibu wa sheria 17 za mchezo wa soka. Lakini haikuwa hivyo ndio maana nimeamua kumkumbusha mwamuzi Ahmed Arajiga na wenzake kwamba mechi wanayokwenda kuchezesha ni dhamana kubwa na ndio inabeba thamani yote ya michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo Azam Media wamewekeza mamilioni ya fedha. 

SOMA NA HII  MENEJIMENTI UWANJA WA MKAPA NI UTUMBO...WANAJUA KUVUNA PESA TU..."KITUNZE KIDUMU"

Wengine wamewekeza kwenye timu na zimetoa ajirakwa wachezaji maelfu.

Waamuzi walioteuliwa kwa ajili ya kucheza mchezo huo ni pamoja na Ahmed Arajiga (Manyara) ambaye atasaidiwa na Ferdnand Chacha (Mwanza) na Mohammed Mkono (Tanga) wakati mwamuzi wa akiba atakuwa ni Elly Sasii wa Dar es Salaam.

Si jambo zuri mtu kufanya uzembe tena kwa zile siasa za kuhofia au kutaka kuwafurahisha baadhi. Au kutaka kutoonekana haukuwa mkatili au haukuboronga na hapa unakuwa umezikanyaga sheria 17 za mchezo wa soka na mwisho lawama kama ilivyo ada zinaangushiwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jambo ambalo si sahihi.

Waamuzi wawe imara na wakumbuke kama watafuata weledi wa kazi yao na uamuzi wao uwanjani ukawa ni ule ambao ni sahihi.

Basi hakuna kitakachoweza kuwaangusha au kuwafanya waonekane walikosea hata kama itakuwa ni baada ya miaka 100 ijayo.

Ukweli haupingiki, ukweli haushindwi milele na vizuri kufanya sahihi na kuacha kuwe na malumbano na kadhalika, lakini mwisho hakuna anayeweza kukushinda.

Bila shaka, hii imekuwa ni tabia kwa muda mrefu kwamba waamuzi wanaingia uwanjani kuchezesha mechi ya watani wakiwa wanataka kuhakikisha inaisha bila kadi nyekundu au kutoa penalti. Wako waamuzi hufurahia hata mechi iishe kwa sare kwa kisingizio cha kupunguza “makelele”.

Suala la “makele” si kazi yao, nani atachukizwa au nani ataumizwa kwa kupoteza au yupi atafurahi kwa kushinda,waamuzi waitoe kabisa hiyo badala yake waende kuchezesha mpira tu na suala la matokeo, litokane na mchezo utakavyokuwa.