Home Makala MENEJIMENTI UWANJA WA MKAPA NI UTUMBO…WANAJUA KUVUNA PESA TU…”KITUNZE KIDUMU”

MENEJIMENTI UWANJA WA MKAPA NI UTUMBO…WANAJUA KUVUNA PESA TU…”KITUNZE KIDUMU”

Uwanja wa Mkapa

TIMU ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inasafiri wiki ijayo kuelekea Kaskazini mwa Afrika kule Misri, kwa ajili ya mchezo wao wa kimataifa wa kundi F wa kufuzu kwa fainali za Afrika, Afcon 2023, dhidi ya majirani zao Tanzania.

Kadhia wanayopata majirani zetu Uganda inaweza kutupata na sisi kama hatutachukua hatua kwa kuongeza nidhamu katika kutunza miundombinu ya viwanja.

Ziara ya hivi karibuni ya maafisa wa CAF iliibua wasiwasi kuhusu hali ya sehemu ya kuchezea (pitch) katika uwanja huo.

Ilishauriwa kupunguzwa kwa michezo inayofanyika katika uwanja huo.

Kufuatia ushauri huo,michezo ya ligi kuu inayozihusu Yanga na Simba iliondolewa katika Uwanja wa Mkapa na hivyo vilabu husika kulazimika kutafuta viwanja vingine kwa baadhi ya michezo yao ya Ligi kuu na kubaki kutumia uwanja wa Mkapa kwa mashindano ya CAF na pia mchezo wa marejeano kati ya Taifa Stars na Uganda.

Tangu uwanja uanze kutumika,nakumbuka katika mechi ya kwanza kulikuwa na malalamiko ya uharibifu na wizi wa vifaa vya maji na umeme.

Upungufu wa nidhamu katika utunzaji wa viwanja unaweza kuwa upande wa watumiaji lakini wajibu ni wa menejimenti.

Watendaji wa uwanja wanatakiwa kujua kuwa matunzo ya uwanja,hasa sehemu ya kuchezea,si ya lelemama.

Nyasi zinahitaji chakula,zinahitaji maji ya kunywa na kuoga,zinahitaji kupumzika na zinahitaji kukatwa au kupunguzwa kwa utaratibu wa kitaalam.Hiki ni kiumbe hai.

Tukiangalie Wembley ulioko Uingereza na ulianzishwa mwaka 1923.

Uwanja huo unameza watazamaji 90,000 waliokaa ukimilikiwa na chama cha mpira (FA) na kuendeshwa na Kampuni ya Wembley National Stadium Ltd.

Tangu mwaka 2022 iliamuliwa kwamba kwa mwaka uwanja utakuwa mwenyeji wa matukio 46 tu.Kati ya matukio hayo 24 ni yale yasiyo ya kimichezo na 22 ni ya kimichezo basi.

Wanawezaje kuenenda na mpango huo? Jibu,nidhamu.

Tukirudi hapa nyumbani,matumizi ya uwanja wa mkapa na viwanja vingine vya michezo yamekosa nidhamu na weledi.

Yeyote,wakati wowote anaweza kuutumia uwanja kadri anavyotaka.

Mara ngapi ratiba ya michezo ya ligi imekuwa ikibadilishwa ili kupisha tamasha,ibada nk.?

Tuko tayari kuitoa kafara kesho endelevu kwa ajili ya pesa za tamasha au kufurahisha watu au kikundi Fulani katika jamii.

Wakati serikali imeeleza adhima yake ya kuongeza miundombinu ya michezo,ni jukumu la wamiliki,iwe ni serikali,halmashauri,Chama cha Mapinduzi na taasisi nyingine binafsi kuimarisha nidhamu katika kutunza miundombinu ambayo tunayo tayari.

Bila kujenga nidhamu ya utunzaji,ujenzi wa viwanja vipya itakuwa ni kumwaga maji kwenye pakacha.

Tutajenga viwanja vingi lakini tusipojenga nidhamu yatatupata ya Uganda na juhudi za Hayati Mkapa aliyepambana kuhakikisha tunajenga uwanja wenye hadhi ya michezo ya daraja la kwanza la FIFA zitakuwa zimepotea bure.Waswahili wanasema “kitunze kidumu”

SOMA NA HII  MBRAZIL "SIMBA YA ROBO NI MOTO BALAAA...USAJILI MPYA YANGA WAITIKISA MAZEMBE