Home Makala USAJILI UNAHITAJI AKILI UKIZUBAA UNAPIGWA

USAJILI UNAHITAJI AKILI UKIZUBAA UNAPIGWA


 TAYARI mambo yanazidi kupamba moto kwenye masuala ya usajili kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2021/22. Bingwa ashajulikana ambaye ni Simba na zile nne ambazo zimeshuka zimefahamika.

Anza na Ihefu pamoja na Gwambina hizi zilikuwa zina msimu mmoja wa kazi na mmoja umetosha kuwarejesha ambapo walikuwa huko Ligi Daraja la Kwanza. Kazi wanayo kwa ajili ya kuweza kurudi tena ndani ya ligi.

Mwadui FC na  JKT Tanzania hawa walikuwepo muda kidogo lakini bahati haikuwa yao wanakazi nyingine ya kufanya kwa ajili ya kuweza kurudi ndani ya ligi.

Kazi ni moja kwao kupambana kutimiza majukumu yao kwa kuwa wakati uliopo ni sasa na kikubwa ni maandalizi mazuri na kufanya kazi kwa ushirikiano.

Mpaka sasa kwa timu ambazo zimejipanga kufanya usajili ninaona kwamba zimeweza kufanya kile ambacho zinahitaji jambo ambalo katika hilo sina mashaka nalo.

Jambo la msingi ambalo linapaswa kuzingatiwa katika usajili ambao unafanywa ni kufuata ripoti ya mwalimu, yeye ndiye ambaye anajua kwamba anahitaji aina gani ya wachezaji kwenye kikosi chake.

Wapo wale ambao watafanya usajili kwa kufuata mahitaji yao hilo lipo wazi kwa kuwa ni mambo ambayo yapo kwenye soka letu la Bongo.  Zama hizo muda wake umekwisha halipaswi lipewe nafasi kwa sasa.

Muda wa kufanya kazi kwa utaalamu na kufuata taaluma ya kazi ya mpira ni sasa. Soka letu linazidi kukua kwa kasi ikiwa masuala ya kufanya maamuzi kwa kuwa wewe ni kiongozi haileti picha nzuri kwa afya ya soka letu.

Timu zote ambazo zitafanya usajili kwa mapendekezo yao binafsi wakati wa kujua masuala hayo yanakuja,  mchezo wa mpira hauhitaji mambo mengi zaidi ya vitendo na data ambazo zinaongea ukweli muda wote.

Ndani ya dakika 90 ni muda sahihi uwanjani ambao utatosha kuaminisha mashabiki na wanachama wa timu kwamba huyo aliyeletwa ndani kucheza ni pendekezo la kocha ama kiongozi.

Sababu moja kubwa itakayofanya atambulike kwamba alisajiliwa kwa presha ama chaguo la kiongozi ni muda wake atakaoutumia ndani ya uwanja na kile ambacho atakionyesha pia pale atakapopata muda.

Ipo wazi kwamba kuna wale wachezaji ambao walipata nafasi ya kusajiliwa kwa msimu wa 2020/21 ndani ya timu mbalimbali hawakuwa na nafasi kwenye timu zao mpaka msimu unaisha.


Namba hazidanganyi kwani wapo wachezaji ambao wamecheza mechi 10 na zote walianzia benchi na hata pale ambapo walianza kikosi cha kwanza hawakumaliza dakika zote 90.

Hii ni mbaya na inatoa picha kwamba hakukuwa na chaguo la mchezaji huyo ndani ya kikosi, pia inaua uwezo wa mchezaji na kurudisha nyuma maendeleo ya soka hasa ikiwa alichukuliwa kutoka kwa timu ambayo ilikuwa inahitaji huduma yake labda kutokana na uchumi kuyumba wakashindwa kubaki na mchezaji.

Kwa viongozi wa timu pia ni somo kwamba mpira wa sasa unahitaji fedha na uwekezaji mkubwa hivyo wanajukumu la kuongeza vyanzo vyao vya mapato ili kuweza kubaki na wachezaji ambao wanawahitaji pale msimu unapokwisha.

SOMA NA HII  KISA USAJILI MPYA SIMBA...KASSIM DEWJI AFUNGUKA MAZITO...AWATAJA CHAMA, LUIS NA 'FEI TOTO'..

Tukiachana na timu na mchezaji pia ana kazi ya kuangalia nafasi yake kule anakokwenda asifikirie kupata mkwanja huku nafasi yake ya kucheza akiiweka kapuni itampoteza kwenye ramani ya mpira.

Kwa kuwa maisha ya soka lazima yaendelee mchezaji mmoja kutoka na kwenda kwenye timu nyingine ni muda sahihi wa kila mchezaji ambaye anakwenda kuanza maisha mapya.

Imani yangu ni kwamba mpaka pale dirisha la usajili litakapofungwa kila kitu kitakuwa kimekwenda sawa ndani ya timu zote kuanzia zile za Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la Pili,Ligi ya Wanawake pamoja na zile zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Umakini unahitajika kwenye usajili ikiwa utazubaa kupigwa ni kawaida kwani zipo timu ambazo zilisajili wachezaji kwa maneno kibao ila wakafeli kufanya vizuri.

Kila mtu atavuna kile atakachokipanda ndani ya uwanja ni wakati wa kuanza maandalizi kwa timu zote kwani muda wa ligi kuanza upo njiani na muda wa dirisha la usajili kufungwa upo karibu.

Ujumbe wangu kwa timu ambazo zimepanda daraja kwa msimu wa 2020/21 zikiwa na uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 zinapaswa zijipange kwelikweli kuleta ushindani.

Geita Gold na Mbeya Kwanza ziwatazame ndugu zao Gwambina na Ihefu namna mambo yalivyokwenda kwao. Pia waitazame Dodoma Jiji ambayo imefanya vizuri ndani ya ligi ikiwa ni msimu wake wa kwanza.

Wakumbuke kwamba ilikuwepo Singida United,Lipuli FC,Ndanda FC,Alliance na Mbao hizi zilidunda kwenye ligi zikashuka Ligi Daraja la Kwanza. Upepo ukakutana nao tena kuna nyingine zipo Ligi Daraja la Pili na Singida United ilishushwa madaraja mawili chini.

Yote kwa yote wasisahau kwamba makosa makubwa ya timu kupata ushindi ni kwenye maandalizi na usajili hivyo wanapaswa kuwa bora katika usajili wakati huu ambao unaelekea ukingoni pamoja na kuanza maandalizi mapema kujenga timu zao.

Muhimu ni kufanya maandalizi mazuri hasa kwa wachezaji ambao watasajiliwa kwa wakati huu. Jambo jingine ni kuweza kuwekeza kwa vijana wao ambao walipanda nao ili waweze kuwapa matokeo baadaye.

Lakini licha ya kumaliza kufanya usajili mzuri ni muhimu kuwa na mpango kazi makini utakaofanya timu iwe inapata matokeo uwanjani na kuleta ushindani kama ilivyokuwa ndani ya Ligi Daraja la Kwanza.

Tunataka kuona kila timu inafanya maajabu na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote ambazo watacheza iwe nyumbani ama ugenini muhimu kupambana kupata matokeo.

Muda wa kufikiria kwamba bado mpo Ligi Daraja la Kwanza umekwisha kwa sasa ni mapambano ndani ya Ligi Kuu Bara ni muhimu kuweka dira mapema kabla mambo hayajaanza kubadilika.

Mashabiki wenu mtambue kwamba wanajua yapo matokeo matatu, kufungwa, sare na kushinda. Furaha yao kubwa ipo kwenye kushinda basi pambaneni kuwapa mashabiki kile ambacho wanahitaji.

Tunahitaji kuona kwamba msimu wa 2021/22 mnakuja kuleta kitu kipya ambacho ni ushindani bila kujali kwamba mmetoka kumaliza maisha yenu ndani ya Ligi Daraja la Kwanza bado mna nafasi ya kufanya vizuri.