MOJA ya wasakata soka ghali kwa upande wa wanawake, huwezi kumuweka kando Pernille Harder ambaye anakipiga ndani ya Klabu ya Chelsea.
Aliletwa duniani Novemba 15,1992 ni raia wa Denmark ambapo kwa sasa ana umri wa miaka 28 na bado anawaka akiwa uwanjani.
Wajihi wake upo sawa na tabasamu lake ni murua hasa pale anapomaliza kazi yake ya kumtungua kipa wa timu pinzani.
Nafasi yake uwanjani ni kiungo mshambuliaji pia anacheza nafasi ya ushambuliaji bila matatizo na anavaa jezi namba 23 ndani ya kikosi cha Chelsea.
Dau lake kutoka Klabu ya Wolfsburg linatajwa kuwa ni Euro 250,000 ilikuwa ni Septemba Mosi,2020 Harder alisaini Chelsea kwa dili la miaka mitatu na alipokutana na timu yake ya zamani katika UEFA Women’s Champions League aliwatungua mabosi wake wa zamani.
Amecheza jumla ya mechi 35 ndani ya Chelsea kwa msimu wa 2020/21 nyota huyo ambaye ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili ule wa kulia na kushoto awapo uwanjani.
Katika mechi hizo amefunga jumla ya mabao 16 na pasi tatu akiwa ameonyeshwa kadi moja ya njano na mara nane aliweza kufanyiwa mabadiliko katika mechi ambazo alianza na 15 alitokea benchi huku akiwa ameyeyusha jumla ya dk 2,347.
Katika timu yake ya taifa ya Denmark, msimu wa 2021 alicheza jumla ya mechi 14 alitupia mabao 9 pasi tatu za mabao bila kuonyeshwa kadi ya njano wala nyekundu huku alianza kikosi cha kwanza mechi 14 na alifanyiwa mabadiliko katika mechi 5 na aliyeyusha jumla dk 1,156.