Home news A-Z KILICHOJIRI UCHAGUZI TFF, TANGA

A-Z KILICHOJIRI UCHAGUZI TFF, TANGA


HATIMAYE Shirikisho la Soka Tanzani,(TFF) limefanikiwa kufanya mkutano mkuu wa mwaka, mkutano ambao uliambatana na na uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

 

Uchaguzi ambao ulilenga kupata Rais na Wajumbe wa Kamati Tendaji ya TFF watakaokaa madarakani kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

 

Uchaguzi huo ulifanyika wikiendi iliyopita siku ya Jumamosi jijini Tanga kwenye hoteli ya Tanga Beach Resort.

 

Championi Jumatatu iliweka kambi kwenye jiji hilo la watu wakarimu na wacheshi kila wakati kwa ajili ya kukuletea msomaji kilicho bora.

 

Ilikuwa ni siku moja kabla ya uchaguzi huo wajumbe 81 kutoka kwenye kanda sita, sawa na mikoa 23 waliwasili jijini Tanga na kupata nafasi ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Michezo eneo la Mikanjuni.

 

Mradi ambao unajengwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA ukisimamiwa na TFF. Ujenzi huo unahusisha viwanja mbalimbali vya michezo, hosteli, Gym, viwanja vya mazoezi, ofisi, nyumba ya umeme na mambo mengine.

 

Kwa mujibu wa Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Alpha Nestory alisema ujenzi huo upo kwa awamu na awamu hii ya kwanza inahusisha viwanja vinne vya mazoezi, viwili vikiwa vya nyasi bandia na nyasi za asili.

 

Mabweni ya wachezaji na viongozi, nyumba ya umeme na ofisi. Huku awamu zingine zikihusisha hoteli, maduka na mambo mengine.

 

Nestory alisema awamu hii ya kwanza wanatarajia kuikabidhi Oktoba 24 mwaka huu.

 

Turudi kwenye uchaguzi wenyewe

 

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Solomon Kibamba. Kibamba hivi karibuni alichaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega.

 

Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima aliyemwakilisha Mbunge wa Mbeya Mjini na Makamu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.

 

Malima alipata nafasi ya kufungua mkutano kwa kutoa hotuba fupi, kubwa akiwapongeza TFF kwa mambo makubwa ambayo wameyafanya kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

 

“Nipo hapa kumwakilisha  Dkt Tulia Ackson ambaye alitakiwa kuwa mgeni rasmi, kutokana na majukumu kuwa mengi akaomba nimwakilishe.

 

“Nawatakia kila kila la heri kwenye uchaguzi huu, lakini pongezi zangu kwa TFF kwa mazuri na makubwa waliyofanya kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.”

 

Mara baada ya Malima kuzungumza ulikuwa wakati wa Karia kuzungumza kile ambacho alifanya kwa kipindi cha miaka minne akiwa Rais, ambapo alisimama akiwa kama mwenyekiti wa mkutano mkuu.


 

Karia alizungumza mafanikio makubwa ambayo aliyapata kwenye kipindi chake ikiwemo kufanikiwa kwenye timu za taifa ikiwemo kwenda Afcon na CHAN, timu za wanawake kutwaa mataji ya Cecafa na COSAFA.

 

Kupata dili mbalimbali za matangazo na ufadhili kwenye ligi, ikiwemo haki za matangazo ya televisheni kutoka Azam TV na matangazo ya redio kutoka TBC, nidhamu ya uongozi na weledi kwenye usimamizi wa fedha na ushirikiano na vyombo vya habari.

 

“Kimsingi tumefanikiwa kufanya mambo mengi kwenye kipindi cha miaka minne iliyopita, ligi zetu zimepiga hatua sana na kupata uwakilishi wa timu nne kwenye mashindano ya kimataifa.

SOMA NA HII  ISHU YA NAMUNGO NA KOCHA MPYA IMEKAA HIVI

 

“Timu zetu za taifa, wanawake na wanaume zimekuwa zikifanya vizuri, tumetengeneza weledi na uwazi kwenye uongozi wetu pamoja na ushirikiano na wanahabari.

 

“Ushirikiano na FIFA pamoja na Caf umekuwa mkubwa zaidi kwa kipindi hiki cha miaka minne, lakini pia tumeweza kupanua miundombinu ya michezo kwenye maeneo ambayo awali mpira ulikuwa hauchezwi.”

 

Upigaji kura

Kwa upande wa kiti cha urais hapakuwa na ugumu, Kibamba alisimama na kuhakikisha kama wajumbe wote 83 walikuwepo na kisha akatoa muongozo wa nini kinatakiwa kufanyika.

 

Aliwakumbusha wajumbe kuwa ibara ya 19 inasema kama mgombea atakuwa mmoja, atapigiwa kura ya ndio au hapana na kisha ibara ya 15 inasema kamati itathibitisha.

 

Kwahiyo Karia akapigiwa kura za ndio na hakukuwa na kura ya Hapana hata moja na kupita kwa ushindi wa asilimia 100.

 

Uchaguzi wa Wajumbe

 

Jumla ya kanda zilikuwa sita na wajumbe wakiwa 17. Kanda hizo ni ile namba moja ya mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani, kanda namba mbili ina mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.

 

Kanda namba tatu ni mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe. Kanda namba nne ina mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida na kanda namba tano ina mikoa ya Geita, Mara, Mwanza na Kagera.

 

Huku kanda namba sita ikiunganisha mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora.

 

Wagombea wote kabla ya uchaguzi walipewa nafasi ya kuomba kura kwa dakika tatu na baada ya hapo uchaguzi ukafanyika wa kuwapa wajumbe sita.

 

Kimsingi Wajumbe wa Kamati Tendaji ya TFF wanatakiwa kuwa 10, lakini kanuni inasema rais atachagua wajumbe wanne mmoja akiwa mwanamke kwenda kutengeneza idadi ya watu 10.

 

Matokeo ya Wajumbe

 

Kura zikapigwa na matokeo yakawa kama yafuatayo.

 

Kanda namba moja mshindi ni Lameck  Nyambaya akipata kura 40, huku Athumani Kambi kura sita sita na Osea Lugano akipata kura 35.

 

Kanda namba mbili mshindi ni Kharid Abdallah Mohamed kwa kura 55, Zakayo Mjema alivuna kura 26

 

Kanda namba tatu mshindi ni James Mhagama kura 46, Abuu Sufian Silia alipata 27 na 

Mohamed Mashandu akavuna kura nane.

 

Kanda namba nne Mohamed Aden ndiye mshindi kwa kura 52, Osuri Kusuri  kura 20 na Hamis Juma Kitila kura nane alipata.

 

Kanda namba tano mshindi ni Vedastus Lufano kwa kura 35,  Salum Umande Chama akapata kura 32 na Salum Kulunge alivuna kura 14.

 

Kanda ya sita na ya mwisho mshindi ni Issa Mrisho Bukuku kwa kura 58, Kenneth Pesambili kura 11 na Bras Kihondo naye akapata 11. 

 

Majina ya wajumbe wanne waliopendekezwa na Rais kwa mujibu wa katiba ni Athumani Nyamlani wa Dar, ambaye aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Wengine ni Ahmed Mgoi wa Kigoma, Hawa Mniga wa Dar na Said Sud kutoka Tanga.