Home Makala VIWIKO NDANI YA UWANJA MUDA WAKE UMEISHA

VIWIKO NDANI YA UWANJA MUDA WAKE UMEISHA


IMEKUWA kawaida kwa sasa wachezaji kupewa adhabu kutokana na ugomvi wanaoonyesha ndani ya uwanja. Sio kwa msimu huu ambao umemeguka hata ule uliopita mambo yalikuwa namna hiyo.

Katika hilo kwa wakati huu wa maandalizi ya msimu ujao ni lazima kila mchezaji aweze kulifanyia kazi ili kusiwe na makosa ya kujirudia kwani muhimu kila kitu kiende sawa.

Ugonjwa huu umekuwa ni wa kuambukiza na matukio haya hayajengi kwa familia ya michezo. Ngumu kuamini wakati mwingine matendo haya yanafanyika na wachezaji ambao ni wale wanaotoka nje ya nchi. Hii haileti picha nzuri.

Hali hiyo pia ilikuwa inaonekana mpaka kwa mashabiki nao kuwa na kasumba ya kuhitaji kugombana pale ambapo mambo yanakuwa yamekwenda kinyume na wanavyofikiria.

Si kwa Yanga,Simba, KMC, Lipuli mpaka Njombe Mji unaambiwa kote kumekuwa na ubabe kwa wachezaji jambo ambalo sio zuri kwa afya ya mpira.

Hivi karibuni kwenye mchezo wa mwisho wa kufungia msimu wa Kombe la Shirikisho ambapo ilikuwa ni fainali tulishuhudia mambo tofauti kutoka kwa wachezaji, mashabiki na viongozi pia.

Tulishuhudia baadhi ya viongozi kutoka Simba na wengine wa Yanga wakionekana kugombana getini jambo hilo lilipelekea faini kutoka Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF).

Mbali na ugomvi huo pia mchezaji Tonombe Mukoko yeye alionekana akimpiga kiwiko mchezaji wa Simba John Bocco jambo ambalo sio uungwana.

Hawa ni washkaji na wanajuana kwani walipokutana kwenye mchezo wa ligi Julai 3 Bocco alikuwa na kazi kubwa ya kucheza na Tonombe ambapo alionekana akimchezea faulo katika harakati za kuokoa mpira.

Katika hili Bocco hakuomba radhi ila Mukoko baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho aliomba radhi na mwisho wa siku maisha yaliendelea. Lakini alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na faini ilifuata pamoja na kufungiwa mechi tatu.

Hii ni mbaya kwa wachezaji kuhama nayo na kwenda nayo msimu ujao haitakuwa jambo la kupendeza muhimu kujipanga kwa wakati ujao.

Mpira ni maisha ya wachezaji hivyo kila mmoja ni lazima awe mlinzi wa mwingine ili kudumisha ushirikiano na upendo. Ikiwa mchezaji atamuumiza mshikaji wake anamuharibia ugali wake hiyo sio sawa.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA CAF ...BARBARA AIBUKA NA KAULI HII YA KISHUJAA..WAMOROCCO WAMJIBU KWA DHARAU..

Masuala ya vitisho kwa ajili ya msimu ujao hasa ambao walikuwa wanapata marefa pamoja na mashabiki wengine inapaswa  iwekwe kando jumla jumla.

Ikiwa utapambana kumuumiza mchezaji hapo unamrudisha nyuma. Hata wale wachezaji ambao wapo Ligi Daraja la Kwanza ni muhimu kupambana kwa busara bila kutumia nguvu.

Vurugu na ugomvi sio sawa kabisa ni lazima msimu ujao wenye ushindani na usiwe na manenomaneno. Pia nakumbuka kuna yale mabuti aliyokutana nayo mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi kutoka kwa mshikaji wake Pascal Wawa wa Simba.

Hapa tuliona namna ambavyo wababe hawa walipambana ila mwisho wa siku ukweli ni  kwamba ugomvi haulipi.

Nidhamu ni muhimu na wachezaji wana kazi ya kuwa walinzi kwa wengine kwa wakati ujao.Umakini unahitajika na kila mmoja atimize jukumu lake kwa wakati.