Home news KISA ‘SUB’ YA WAWA…PABLO AWAPIGIA MAGOTI SIMBA…AVUNJA UKIMYA KILICHOTOKEA…

KISA ‘SUB’ YA WAWA…PABLO AWAPIGIA MAGOTI SIMBA…AVUNJA UKIMYA KILICHOTOKEA…


MTU mzima akivukwa nguo huchutama! Ndivyo unavyoweza kusema kwa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco baada ya kuwaangukia wana Simba na mashabiki wa soka kwa ujumla kwa kitendo alichokifanya juzi kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini hapa.

Sio kuomba radhi tu, kocha huyo kutoka Hispania pia alifunguka kilichomfanya apagawe na kufikia kuzuia ‘sub’ ya Paschal Wawa kwa kufikia hatua ya kumsukuma, kupiga chini chupa ya maji na kupiga teke kiti mbali na kukaa chini kwa hasira kwenye mechi dhidi ya KMC.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda mabao 4-1 na kujikita nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Kocha huyo alifafanua juu la tukio hilo lililozua maswali mengi kwa wadau, hasa baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa yeye haivi na wasaidizi wake na pia anajiandaa kumtema Wawa kikosini kwa kusema anawaomba radhi wana Simba na mashabiki wa soka, lakini alipandwa na hasira kutokana na kuzinguliwa na mwamuzi wa akiba kubadilisha wachezaji tofauti na matakwa ya benchi la ufundi.

“Kwanza kabisa ilikuwa tukio ambalo nilipaniki, lakini kwangu ninachotaka kusema ni kwamba mimi kama kocha haina maana ya kwamba napaswa kulielezea. Ila ni kwamba mabadiliko ya wachezaji watano waliopo benchi yanapaswa kufanywa katika mikupuo mitatu,” alisema Pablo.

“Wa kwanza ilikuwa imeshafanyika ya pili nilitaka wachezaji wawili waingie Jimson Mwanuke na Wawa baada ya Mwanuke kuingia refa aliruhusu mchezo uendelee huku Wawa akiwa nje. Ndio maana nikawa na hasira kwani katika maisha yangu ya mpira sijawahi kuona kitu kama hiki kwa maana mabadiliko ya wachezaji wawili anaingizwa mchezaji mmoja.”

Pablo aliongeza kuwa, “kwa mara ya tatu niliomba kufanya ‘sub’ nyingine ya mwisho ambapo tulitaka Abdulswamad Kassim na Pascal Wawa waingie badala ya Mohammed Hussein na Henock Inonga, refa akarudia kosa lilelile baada ya Abdulswamad kuingia aliruhusu mchezo kuendelea.

“Licha ya hayo naomba nikiri nilivyohamasika haikuwa sawa kwa faida ya klabu yetu yenye taswira nzuri kwa Jamii japo nilikuwa na hasira. Ninaomba msamaha kwa watu wote waliokuwa wanaangalia mchezo na waliokuja uwanjani – watoto kwa wakubwa na kwa marefa.

SOMA NA HII  UNAAMBIWA HUYO AYOUB WA SIMBA BADO HAJAANZA BALAA LAKE

“Makosa ya kibinadamu yaliyotokea ikumbukwe mimi nawakilisha klabu kubwa. Napaswa kuwa mfano kwa wengine kwa mazuri na sio mabaya. Ninaomba mnisamehe kwa kilichotokea kama kocha sikupaswa kufanya vile mbele ya mashabiki mbalimbali waliokuja kutusapoti katika mchezo wetu dhidi ya KMC.”

Pablo aliongeza: “Huo ndio ukweli wa kilichotokea sio kama watu wanavyoongea kuwa kocha msaidizi, Seleman Matola na meneja Patrick Rweyemamu walitaka kuweka mchezaji wao, ambao sikuwataka.”