Home Habari za michezo MASTAA WAIWEKA SIMBA MTEGONI…TRY AGAIN ASHINDWA KUJIZUIA..ATAJA ‘VIFAA VIPYA’ VITAKAVYOSHUKA…

MASTAA WAIWEKA SIMBA MTEGONI…TRY AGAIN ASHINDWA KUJIZUIA..ATAJA ‘VIFAA VIPYA’ VITAKAVYOSHUKA…


WACHEZAJI sita wa Simba wanatarajia kumaliza mikataba yao kwenye klabu hiyo huku kuendelea kubaki au kutobaki kutatokana na ripoti ya Kocha Mkuu, Pablo Franco.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa wachezaji Bernard Morrison, Chris Mugalu, Meddie Kagere, Thadeo Lwanga, Joash Onyango na Paschal Wawa mikataba yao inaelekea ukingoni, huku ikitajwa klabu ipo kwenye mazungumza na baadhi ya wachezaji ambao inataka kuwabakisha.

“Tunajua kuna baadhi ya wachezaji wanakaribia kumaliza mikataba yao, lakini tuko kwenye mazungumzo nao, na kubaki au kutoendelea pia kutatokana na ripoti ya mwalimu,” alisema Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally.

Hata hivyo, wachezaji Mugalu na Wawa ndiyo kwa kiasi kikubwa wanaonekana huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea kupisha wachezaji wengine wa kigeni kusajiliwa.

Wawa ambaye msimu uliopita nusura aachwe, aliongezwa mkataba wa mwaka mmoja, huku Mugalu akionekana kuwa zaidi kwenye chumba cha matibabu badala ya uwanjani.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema kuwa watasajili wachezaji wanne wa kigeni wenye uwezo wa hali ya juu, ili kukiboresha kikosi hicho na kuwa imara kwenye msimu ujao wa michuano ya kimataifa.

Alisema wanatarajia kusajili beki mmoja wa kati, mastraika wawili na winga mmoja.

Pamoja na kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika hatua ya makundi, lakini baadhi ya wanachama na mashabiki wamekuwa hawaridhishwi na kiwango cha timu hiyo msimu huu.

Wamekuwa wakidai baadhi ya wachezaji wageni na wazawa viwango vyao vimepungua, hivyo kunahitajika usajili wa nguvu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, kuirudisha Simba ile ambayo imezoeleka kuwa tishio kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baadhi ya wachezaji wanaotajwa kufikia mahali pazuri kwenye usajili ni Victorien Adebayor anayeichezea US Gendamarie ya Niger na Moses Phiri anayechezea Zanaco ya Zambia.

SOMA NA HII  SAKATA LA YANGA NA FEI TOTO.....GEOFF LEO NAYE 'AINYEA' TFF.....AITAJA FIFA....