Home Habari za michezo KWA MIGOLI HII YA KUMWAGA ALAFU YANGA ASIWE BINGWA..?ALLY MAYAI KAONA ISIWE...

KWA MIGOLI HII YA KUMWAGA ALAFU YANGA ASIWE BINGWA..?ALLY MAYAI KAONA ISIWE TABU KAFUNGUKA HILI..


YANGA msimu huu kila sehemu ni tamu. Ukiachana na kuongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi, umiliki wa mabao yao 29 una vionjo vya kusisimua kwa namna yalivyofungwa kwa staili tofauti.

Achana na mabao hayo (29) kufungwa na safu zote kasoro kipa, aina ya ufungaji umekuwa wa aina yake kwani yapo ya nje ya 18, mipira ya kutenga, frii-kiki na penalti.

Gazeti la Mwanaspoti limechambua na kueleza namna mabao hayo yalivyopatikana kwa njia ya data kutokana na msimamo wa ligi.

PENALTI (3)

Yanga ilifunga dhidi ya Ruvu Shooting, alipiga beki Shaban Djuma katika dakika ya 18, ilitokana na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuchezewa rafu na Ally Sonso (sasa marehemu), nyingine ilipigwa Said Ntibanzonkiza ‘Saido’ dhidi ya Namungo dakika ya 90 na ya tatu alipiga Saido dhidi ya Biashara United dakika ya 79, ilitokana na Jesus Moloko kuchezewa rafu na beki AbdulMajid Mangalo.

Mabao YA FRII-KIKI (2)

Mabao mawili ya mipira ya adhabu ndogo yaliwekwa wavuni na Saido dhidi ya Mbeya Kwanza katika dakika ya 18, baada ya Fei Toto kuchezewa rafu nje ya 18, Saido alipiga mpira wa kutenga nje ya 18 ambapo Fiston Mayele aliunganisha kwa kichwa dakika ya 51 dhidi ya Kagera Sugar.

MABAO YA KICHWA (4)

Kiungo mkabaji Khalid Aucho alikuwa wa kwanza kufunga bao la kichwa dhidi ya Tanzania Prisons akipokea krosi ya Saido katika dakika 44, huku matatu yakifungwa na Mayele dhidi ya Coastal Union katika dakika 40, Kagera Sugar dakika 30 na 51, krosi zote mbili zilitoka kwa Saido, katika mchezo huo wa Mkwakwani, Yanga ilishinda mabao 3-0.

NJE YA 18 (5)

Pazia la mabao ya aina hii lilifunguliwa na Fei Toto katika mchezo wa tatu wa Ligi Kuu kwa kumtungua kwa shuti kali golikipa wao wa zamani Farouk Shikalo dakika ya 11, kisha akafanya hivyo tena Kwa Mkapa dhidi ya Ruvu Shooting katika dakika ya 32 kwa kuunganisha mpira uliodondoka nje ya boksi. Mabao mengine ya aina hiyo yalifungwa na Saido ambaye naye amefunga mawili nje boksi akiwafunga Mbeya kwanza dakika ya 18 na Kagera Sugar dakika ya 65, huku naye Jesus Moloko akifanya hivyo dhidi ya Dodoma Jiji katika dakika ya 56.

Idadi hiyo ya mabao matano nje ya boksi inaonyesha kuwa klabu imefunga mabao mengi zaidi ndani ya 18 ambapo imefunga mabao 24 kitu ambacho kinatoa taswira ya kwamba kikosi hicho cha Nabi kina uwezo mkubwa wa kufika katika eneo la hatari na kuzitumia nafasi wanazozipata.

Mbali na aina hizo za mabao, kuna bao moja la kideoni (tiktaka) ambalo alilifunga Fiston Mayele dhidi ya Biashara United akiunganisha vyema krosi iliyopigwa na Djuma Shabani kutokea upande wa kulia. Bao hili liliwaacha midomo wazi mashabiki waliohudhuria mchezo hapo kwa Mkapa huku wengine wakidai linastahili kuingia kuwania tuzo ya Bao Bora la msimu la Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  FT: DODOMA JIJI 0-1 SIMBA SC....BALEKE AANZA KUJIBU MASWALI MAGUMU...SAWADOGO MHH..

Ukiachana na jinsi ambavyo mafungaji wa mabao hayo walivyowafunga, bado Mwanaspoti linakusogezea njia za mabao hayo yalivyotokea ama unaweza kusema aina ya upishi wa mabao hayo huku likikuonyesha ni maeneo gani yametumika zaidi kutengeneza mabao hayo 29.

Krosi (mabao 8)

Yanga wamekuwa wakitumia sana njia ya krosi kujipatia mabao yao ambapo kufikia sasa ni mabao saba ambayo yametokana na krosi za upendo kutoka kwa mawinga na mabeki wa pembeni ambapo krosi hizi zilizozaa mabao zilipigwa na Yacouba Songne (1), Kibwana Shomari (1), Yassin Mustafa (1), Saido (2), Farid Mussa (1), Djuma Shabani (2).

Lakini pia kikosi hicho kimeonyesha ubunifu wa kutumia pande zote katika kutengeneza mabao hayo ambapo mabao manane yametokea upande wa kushoto huku waliohusika ni Kibwana Shomari, Farid Mussa, Saido Ntibazonkiza, Dickson Ambundo pamoja na Yacouba Songne kabla hajapata majeraha, Mabao matano yametokea uapnde wa kulia ambao waliohusika katika kuchakata mabao hayo ni Djuma Shabani, Moloko na Denis Nkane, huku katika eneo la kati limepika mabao 10 likiongozwa na Feisal Salum ‘Toto’, Khalid Aucho, Salum Abubakari ‘Sure Boy’ na Yanick Bangala.

WASIKIE WADAU

Staa wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema kuwa kuna mabadiliko makubwa ndani ya kikosi cha Yanga ukilinganisha na misimu kadhaa iliyopita jambo ambalo limeleta utofauti mkubwa wa kikosi hicho kilichojaa ubunifu mkubwa wa mabao yao.

“Yanga walianza kuonyesha dalili za kuwa na ubora na kiwango hiki tangu mwazoni mwa msimu na pia napongeza utulivu wao walioufanya kwenye vipindi vya usajili na matokeo yake tumeyaona na kama wakitulia tena kwenye dirisha lijalo basi wanaweza kuongeza moto zaidi,” alisema Chambua.

Naye nyota wa zamani wa timu ya Taifa na klabu ya Yanga, Ally Mayay alisema kuwa matokeo mazuri ya kikosi cha Yanga yanachagizwa na uwezo walionao watu wa benchi la ufundi likiongozwa na kocha Nasreddine Nabi.

“Uwezo mkubwa wa kocha huyu umeleta chachu ya ushindi ambapo kupitia yeye tumeona baadhi ya wachezaji kuongeza viwango huku wengine wakipata bahati ya kuongeza uzoefu mwingine wa kucheza nafasi tofauti ndani ya kiwanja hivyo hata upikwaji wa mabao unaonyesha kuwa ni muda wowote wanaweza kukufunga kama ukikosa umakini,” alisema Mayay.