Home Habari za michezo KUELEKEA KARIAKOO DABI…TAKWIMU ZA MAYELE ZAITISHA SIMBA…AHADI YAKE IKO PALE PALE…

KUELEKEA KARIAKOO DABI…TAKWIMU ZA MAYELE ZAITISHA SIMBA…AHADI YAKE IKO PALE PALE…


FISTON Mayele alitoa ahadi mbili ambazo moja ilikuwa ni kuifunga Namungo FC ambayo ameikamilisha na ya pili ni ya kupachika bao katika mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba itakayochezwa Jumamosi kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Lakini, wakati watu wakisubiri kuona kama mshambuliaji huyo atatimiza ahadi hiyo au la, ameweka rekodi ambayo bila shaka upande wa pili wakiisikia hawawezi kumdharau mshambuliaji huyo na watalazimika kumuandalia ulinzi wa ziada ili asiwaletee madhara.

Rekodi hiyo ya Mayele ambayo sio taarifa nzuri kwa Simba kuelekea mechi baina yao Jumamosi ni ile ya kuhusika moja kwa moja na mabao saba katika michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu ambayo Yanga imecheza kabla ya mchezo huo wa watani wa jadi.

Nyota huyo anayeongoza kwa kufumania nyavu amehusika moja kwa moja na mabao hayo saba ya Yanga katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Geita Gold, KMC, Azam FC na ile waliyokabiliana na Namungo FC.

Mabao matano kati ya hayo, yamefungwa na Mayele ambayo alipachika dhidi ya Mtibwa, Kagera Sugar, Geita Gold, Azam FC na Namungo huku bao moja dhidi ya KMC, likiwa la kujifunga la beki Andrew Vincent alipokuwa katika harakati za kuokoa shuti la mshambuliaji huyo.

Idadi hiyo ya mabao saba ambayo Mayele kaifungia Yanga katika mechi sita ni zaidi ya nusu ya mabao yote 12 ambayo timu yake imeyafunga katika mechi sita zilizopita.

Ukiyaweka mabao hayo ya Mayele katika asilimia, mchango wa mabao ya mshambuliaji huyo katika mechi sita zilizopita ambazo Yanga imecheza kwenye ligi hiyo ni sawa na asilimia 58.33 na wachezaji wengine waliobakia wametoa mchango wa asilimia 41.67.

Takwimu hizo zinamfanya Mayele kuwa mchezaji aliyehusika na idadi kubwa ya mabao katika ligi kwenye mechi sita zilizopita kuliko mwingine yeyote akifuatiwa na George Mpole na Clatous Chama na Medie Kagere wa Simba.

Mpole wa Geita Gold, anashika nafasi ya pili nyuma ya Mayele ambapo katika mechi sita zilizopita, amehusika na mabao manne kati ya mabao sita ya timu yake ikiwa ni sawa na asilimia 66.66

SOMA NA HII  ISHU YA MUKOKO TONOMBE KUEPA YANGA IPO NAMNA HII

Chama na Kagere wamefungana nafasi ya tatu kwa pamoja ambapo kila mmoja amefunga mabao matatu ikiwa ni sawa na asilimia 33.33 ya mabao yote tisa ambayo Simba imepachika katika mechi sita zilizopita za ligi.

Kocha wa Namungo FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema kuwa Mayele ni mchezaji mzuri, “ni mjanja wa kuwakimbia mabeki pale wanaposhambulia hivyo huwa hana masihara ukifanya makosa kwani atakufunga.”