Home Azam FC KUELEKEA MECHI YA LEO…TAKWIMU ZINAONGEA….YANGA WAIZIDI AZAM KIDOOGO…

KUELEKEA MECHI YA LEO…TAKWIMU ZINAONGEA….YANGA WAIZIDI AZAM KIDOOGO…


Azam dhidi ya Yanga daima imekuwa mechi ya kukata na shoka sana iliyojaa ushindani na takwimu zinathibitisha kwamba wapinzani hao hakuna aliye zaidi ya mwenzake, Yaani wote wamekuwa wakimenyana vikali.

Takwimu zinaonyesha kwamba timu hizo mbili zimekutana mara 27 kwenye Ligi Kuu tangu Oktoba 2008, Yanga imeshinda mara 10, Azam imeshinda mara 9 na mara 8 zilizobaki timu hizo zimetoka sare.

Katika mechi hizo Azam imefunga mabao 30 wakati Yanga imefunga mabao 31 na ndio maana katika mechi ya leo hatumwi mtoto dukani.

Yanga imekuwa katika kiwango bora zaidi msimu huu ikiongoza Ligi Kuu Bara kwa alama 48 huku ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu wakati Azam ambayo haikuwa na mwanzo mzuri wa msimu, imeibuka katika siku za karibuni na sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28 baada ya mechi 18.

Lakini kwa kuwa Azam ndiyo timu ya mwisho kuifunga Yanga Aprili 25, mwaka jana, wababe hao wa Jangwani watakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuboresha rekodi yao nzuri ya kucheza mechi 25 za Ligi Kuu bila kupoteza.

Kufikia mechi ya leo Yanga imekuwa na jeuri juu ya safu yake ya ulinzi. Hadi sasa msimu huu, Yanga imeshinda mechi 15 na sare tatu, huku ikiwa imeruhusu mabao machache zaidi (manne).

Licha ya jina la straika wa timu hiyo, Fiston Mayele kutamba kila kona na mabao yake 10, kuna ukuta mgumu, unaompa jeuri Nasreddine Nabi.

Kazi ngumu inayofanywa na mabeki Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Shaban Djuma, Kibwana Shomari, Yannick Bangala na Khalid Aucho, licha ya Yanga kushindwa kuifunga Mbeya City (0-0) na Simba (0-0), waliweka ulinzi mkali wa eneo lao.

Katika mabeki hao, Job amekuwa panga pangua kikosini, mechi 18 amecheza 15, akikosa tatu baada ya kufungiwa na TFF kwa kosa la kumchezea rafu mchezaji wa Mbeya City, Richardson Ng’ondya.

Nabi amekuwa akiwatumia katikati Mwamnyeto na Job, wakati mwingine Bangala akimchezesha na Job, huku pembeni amekuwa akiwabadilisha Kibwana Shomary, Shaban Djuma, wasipokuwepo hao wapo Yassin Mustapha, David Bryson, Farid Mussa na Paul Godfrey.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONEWA 'ROUND' YA KWANZA ...SIMBA NA YANGA ZAANZA KUJIPATA MDOGO MDOGO..

Nabi, alisema anachojivunia ni kuwa na mabeki waliozoeana akiwatolea mfano Mwamnyeto na Job, huku wazoefu Aucho na Bangala wakiongeza nguvu kulingana na uzoefu wao.

“Bangala na Aucho wanasaidia kuondoa makosa, inapotokea mabeki wa kati wakafanya, ila kiujumla timu nzima inapambana na kuhakikisha tunachukua ubingwa,” alisema. Ukiachana na Yanga kuruhusu mabao machache, Simba ndio inayofuatia katika mechi 17 imetikiswa mara sita nyavuni.

Kwa upande wa Azam FC ambao ukuta wao umekuwa ukibadilika mara kwa mara umeruhusu mabao 16 kwenye michezo 18 waliyocheza wakishinda mechi nane, wametoka sare nne na kufungwa sita.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin kwenye safu yake ya ulinzi amekuwa akifanya mabadiliko mara kwa mara kwa kumtumia Paul Katema, Bruce Kangwa, Agrey Morris na Abdallah Heri na muda mwingine amekuwa akiwatumia Lusajo Mwaikenda, Edward Manyama, Pascal Msindo, Daniel Amour. Katika mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Azam timu hiyo imeonekana kuwa na mzuka wa aina yake.